Taasisi ya Red Cross Tanzania kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo wamewatembelea wananchi wa Kata ya Nkuhungu walioathiriwa na mafuriko na kugawa misaada ya takribani Tsh 35,000,000 katika kuwapunguzia makali wananchi waathirika ambao asilimia kubwa wamepoteza makazi pamoja vifaa muhimu katika uendeshaji wa maisha ya kila siku. 


Zoezi hilo liliendeshwa na Rais wa Red Cross Tanzania Mh. David Kihenzile Mwakiposa ambaye alitoa pole kwa wananchi kwa tatizo hili kubwa la mafuriko na kusisitiza kwamba ni malengo makuu  ya Red Cross kusaidia wananchi wahitaji pindi wanapopatwa na matatizo na kuwa sehemu ya faraja,na pia alitoa rai kwa wananchi kujiunga na Red Cross ili kuwa sehemu ya faraja kwa wananchi wanaopatwa na majanga mbalimbali.


“Niwape pole kwa changamoto hii kubwa iliyowapata,nilipokea maombi ya Mbunge wenu Mavunde kuiomba Taasisi yangu kusaidia mahitaji muhimu kama mashuka,magodoro,vyandarua,ndoo na vifaa vya ndani.Hivyo nina furaha kukabidhi vifaa hivi kwa wahitaji na niwatake viongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha zoezi la ugawaji wa vifaa hivi linafanyika kwa haki na kuwafikia walengwa”Alisema Mwakiposa


Akishukuru kwa niaba ya Wananchi,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini *Mh. Anthony Mavunde* ameipongeza Red Cross Tanzania kwa uharaka wake wa kuitikia maombi ya msaada wa vifaa na kuwashika mkono wananchi jambo ambalo limewapa faraja wananchi hao wa Nkuhungu ambao wamekumbwa na mafuriko makubwa ya mvua hali iliyosababisha kuhama makazi yao kutokana na uwingi mkubwa wa maji uliozunguka makazi yao.


Mbunge Mavunde pia alitumia fursa kulishukuru Kanisa Katoliki Parokia ya Nkuhungu kwa msaada wa unga,sabuni na mafuta vitu vyote vikiwa na  thamani ya Tsh 2,500,000


Share To:

msumbanews

Post A Comment: