Na Atley, DODOMA


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo, ametoa siku 12 kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kuhakikisha kero zilizopo katika Soko la Job Ndugai na Stendi ya mabasi ya Dodoma zinatatuliwa.


Jafo ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kutembelea miradi minne ya kimkakati ambapo alionyesha wazi kutoridhishwa na miradi hiyo miwili kwa namna inavyoendeshwa.


Akiwa katika mradi wa Soko la Job Ndugai, Waziri Jafo alionesha kutoridhika na uongozi wa Soko hilo kuwatoza Wafanyabiashara  wenye vizimba kulipa ushuru wa shilingi 70,000 badala ya shilingi 20,000.


Kero nyingine aliyoishuhudia Waziri Jafo ni kitendo cha Malori makubwa ya mizigo kuendelea kushusha na kupakia katika soko la majengo na masoko mengine yaliyopo katikati ya jiji hali inayosababisha malori hayo kuharibu miundombinu ya barabara.


Kufuatia hali hiyo Waziri Jafo ameuagiza uongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha kuwa kuanzia tarehe 10 mwezi huu malori yote makubwa ya mizigo yanashusha na kupakia katika soko la Ndugai.


“Sijaridhishwa na hali ya soko hili nimekuwa Very Dissapointed, naagiza kabla ya tarehe 10 soko liwe ‘busy otherwise’ miradi yote tutakuwa tunapeleka Halmashauri nyingine maana wapo waliohitaji hawajapata lakini cha kushangaza hakuna kinachoendelea hapa,” amesema na kuongeza:


“Nikija tena hapa nikute mizigo inashushwa na magari madogo ya mizigo yachukulie hapa maana huko barabara zimeharibika wakati serikali imeweka maeneo maalum kwa ajili ya kushusha mizigo, Mimi siwaelewi kwa nini ushushaji mizigo Bado unaendelea katikati ya jiji,”amesema.

Waziri Jafo alisema inawezekana jiji hawajajipanga kwakuwa alitegemea akifika eneo hilo akute pamechangamka na malori yanashusha mizigo mikubwa na kwamba wangejipanga hali isingekuwa hivyo.

Kuhusu Stendi ya mabasi, Waziri huyo aliwapa siku mbili uongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha wanaweka Scanner na mashine za kukusanyia mapato za POSS kwa ajili ya  ukusanyaji mapato katika mageti yote na yawe yanafanya kazi ili kila mwananchi awe na uhuru wa kupita anapotaka.


“Viongozi wa mkoa huu nimeridhishwa na utaratibu wa mabasi yote kuingia stendi na abiria kupakiwa na kushushwa hapa lakini changamoto ya matumizi ya geti moja tu ifanyiwe kazi,  angalieni vizuri maana inawezekana kuna mtu maalum kapewa ikiwezekana muwe na vitambulisho,” amesema.


Amemtaka meneja wa stendi hiyo kutoa vitambulisho kwa mawakala wa mabasi wanaofanya shughuli Stendi ili kero ya Suma JKT ya kuwazuia kutumia mageti mengine imalizike


“Meneja wa Stendi na watendaji wengine simamieni askari wanaofanya kazi hapa ili kuondokana na changamoto ya watu kubambikiwa makosa ili watoe fedha maana inaashiria vitendo vya rushwa jambo ambapo sio zuri,” amesema.


Kuhusu mradi wa Chinangali Park ambao mwekezaji wake  aliyejulikana kwa jina la Captown analipa ushuru wa sh. Milioni 18 kwa mwezi alishauri mkataba wake kurekebishwa ikiwezekana uwe wa miaka mitatu badala ya mmoja ili akishindwa kufanya kazi vizuri apewe mtu mwingine.


“Badilisheni mkataba uwe wa miaka mitatu ukiisha kama hajafanya vizuri mchukue hatua maana muda wa mwaka mmoja ni mdogo na hatujui kama kwa muda huo mtu anaweza kuaminika na taasisi za kibenki kukopa, muongezeeni,”amesema.


Kwenye Mradi wa maegesho ya magari Nala, ambao malori zaidi ya 100 kwa sasa yanapaki Waziri Jafo alionyesha kuridhishwa na mradi huo huku akiagiza huduma za kibinadamu kuwekwa eneo hilo ili madereva wapate mahitaji maalum na wawekezaji wahamasishwe kuja kuwekeza.

Akitoa shukrani baada ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binillith Mahenge alimhakikishia Waziri Jafo kuwa changamoto zilizoainishwa na wafanyabiashara zitafanyiwa kazi na maelekezo yaliyotolewa yatatatuliwa ili jiji lipate faida na wananchi wapate huduma.

 MWISHO.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: