Mhandisi kutoka Kampuni ya Silver Crescent.Turkey Organization,  Hadji Mwisakah inayotekeleza ukarabati wa miundombinu ya visima jimbo la Singida Kaskazini aliyevaa shati rangi ya kijivu akiwa na mafundi wengine pamoja na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Sekoutoure akikarabati miundombinu ya kisima cha maji kilichopo kijijini hapo.


Shughuli ya ukarabati wa miundombinu ya kisima katika kijiji cha Sekoutoure ikiendelea.

Kazi ikiendelea,aliyesimama kushoto ni katibu wa Mbunge Haruna Ntandu akiwa sambamba na mafundi na baadhi ya wananchi.Mhandisi Hadji Mwisakah (kulia) akiwa na mwenzake wakinawa baada ya kukamilika ukarabati katika kisima kilichopo shule ya msingi Sekoutoure.
 


Na Boniphace Jilili, Singida


MBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini Ramadhan Ighondo amepania kuondoa changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa jimbo hilo ambapo mpaka sasa amefufua visima 18 na kuchimba visima vipya 2.

Akiendelea na shughuli hiyo na kuhakikisha kila maeneo wakazi wake wanapata huduma ya maji Ighondo alisema lengo lake ni kuondoa kabisa matumizi ya maji yasio safi kwa wananchi wa jimbo hilo.

"Nilifanya ziara ndani ya jimbo langu changamoto kubwa ni maeneo mengi wananchi wanatumia maji ya kwenye madimbwi ambayo hata wanyama wanatumia,jambo hilo lilinihuzunisha ndio maana nikaona nianze na hili. Mpaka sasa nimekarabati visima 18 nimechimba visima vingine vipya 2  na bado tunaendelea na ukarabati." alisema Ighondo.

Aidha licha ya Serikali na wadau mbalimbali kujenga miradi mingi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa urahisi lakini bado wananchi na baadhi ya viongozi wa ngazi za chini hasa katika Jimbo la Singida Kaskazini hawaithamini na kuitunza miradi hiyo.

"Serikali yetu imechimba visima lengo ni wananchi wapate maji,visima vingi vimeharibika kwa kukosa usimamizi, niwaombe viongozi wa Serikali za Vijijini kuiangalia miradi hii kwa ukaribu na kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaoharibu miundombinu ya miradi hii." alisema Ighondo.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwahango iliopo Kata ya Ilongero,  Elia Andrew alisema shule hiyo inakisima cha maji lakini kwa mda mrefu kiliharbika hivyo wanafunzi walikuwa wanafuata maji umbali mrefu kwa ajili ya kufanyia usafi hapo shuleni na kupelekea wakati mwingine kuchelewa masomo.

 Mwenyekiti wa Kijiji cha Makhandi, Juma Mwanga ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyochimbiwa visima vipya alisema licha ya kuwepo visima vingine lakini kisima hicho ni kikubwa ambacho kitawahudumia wananchi wote wa kijiji hicho ambao ni zaidi ya wakazi 1,200.

"Kwa kweli tunamshukuru sana mbunge kwa jitihada zake za kutuletea maji, ametimiza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi kwa mda mchache huu toka aingie madarakani,tunaomba aendelee na maeneo mengine ambayo yanachangamoto ya maji."

Katibu wa Mbunge,  Haruna Ntandu alisema ukarabati unaoendelea wa visima ni pamoja na kubadilisha mifumo ya utoaji maji kutoka mashine za kujaza (Pamp) na kufunga mfumo wa umeme na jenereta ambapo pia zoezi hilo ni endelevu.

Kwa sasa vibaumbele vya Mbunge Ramadhan Ighondo katika kuwatumikia wananchi wake ni Maji, Afya pamoja na Elimu.

Share To:

Post A Comment: