Na Mwandishi wetu, Kiteto

MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amewaasa Madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, kuepuka vitendo vya rushwa viliyotafsiriwa kwa vitendo 24.

Makungu akizungumza na madiwani na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto amesema vitendo hivyo 24 vipo kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Amesema ni kosa kwa mtu yeyote au wakala wake kutumia nyaraka kwa lengo la kudanganya na kujipatia fedha au faida kwenye shughuli za mwajiri wake zikiwa na maelezo ya uongo, potofu au kasoro yoyote.

"Tumeona katika kipindi kilichopita baadhi ya madiwani walilazimisha kulipwa posho za kujikimu, posho za kujikimu msingi wake ni diwani awe amesafiri na kulala nje ya makazi yake ili kuhudhuria mkutano siku inayofuata kwa hiyo akibainika hatua zitachukuliwa chini ya kifungu hicho," amesema Makungu.

Amesema wapo baadhi ya wakuu wa idara wanaoandaa vikao hewa, ukumbi hewa, kisha wanawalipa washiriki hewa wa vikao au mikutano hiyo na wanadai malipo baada ya kupata stakabadhi na pia wengine wanaandaa miradi hewa ukifika sehemu husika haipo.

Amesema wapo baadhi wanaandaa safari hewa kwa kuonyesha kuwa walisafiri na kutaka malipo ili hali wanatambua kuwa hawakusafiri kwenda popote.

"Madiwani mnayo majukumu ya kubaini hayo yote na kuyatolea maazimio ya haki kwenye vikao vyenu kwa manufaa ya wananchi mnaowawakilisha," amesema Makungu.

Amesema katika halmashauri kuna manunuzi ya huduma mbalimbali kama mafuta ya magari na vifaa mbalimbali ambapo bei hukuzwa pengine hata mara mbili ya bei yake halisi.

"Kwenye pembejeo za kilimo nyaraka za udanganyifu pia hutumika kwani wapo baadhi ya maofisa kilimo hutumia majina ya marehemu kupitia mawakala ili wapate pembejeo na madiwani wapo kwenye kata wanashindwa kubaini hilo," amesema Makungu.

Amesema ni kosa kwa mtu yeyote kutumia madaraka yake huku akivunja sheria katika kutekeleza au kuacha kutekeleza majukumu yake ya kiofisi kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyo halali yeye mwenyewe au mtu mwingine.

Amesema sheria inaweka katazo kwa watakaotumia udiwani kujipatia ukandarasi wafahamu  watakumbana na TAKUKURU kama sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 inavyoelekeza.

Amesema TAKUKURU ni kiongozi wa mapambano ya rushwa hata hivyo kila mwananchi anawajibika katika vita dhidi ya rushwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 27 (2).

"Ibara hiyo inasema watu wote wanatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za ubadhirifu na uharibifu na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa Hali ya baadaye ya Taifa lao." Amesema Makungu.
Share To:

Post A Comment: