Na Mwandishi Wetu, Mwanza  


Serikali yazitaka halmashauri zote nchini kusimamia na kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwenye Vituo vya kutolea huduma za afya ili kuondoa utegemezi kwa serikali kuu na wahisani wa maendeleo.


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.


Katika ziara yake Dkt.Dugange ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuchangia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.4 fedha kutoka mapato ya ndani kwenye ujenzi, ukarabati na upanuzi wa wodi za hospitali, vituo vya afya, na zahanati vilivyopo katika jiji hilo.


“Natoa wito kwa Halmashauri zote kuiga mfano huo kwa kutenga fedha kutoka mapato ya ndani ili kuanza kununua vifaa tiba vitakavyowezesha vituo vya afya vipya vilivyojengwa kwa fedha nyingi za serikali kuanza kutoa huduma kwa wananchi badala ya kuwacheleweshea huduma wananchi”, ametoa wito Dkt.Dugange


Katika hatua nyingine Dkt. Dudange amesema kuwa amevutiwa na ubunifu uliofanywa na uongozi wa Jiji la Mwanza wa kutumia mapato ya ndani kuwahudumia wananchi wake kwa kutoa kipaumbele kwa huduma za afya. 


Dkt.Dugange amekagua ujenzi na ukarabati wa Zahanati ya Fumagila iliyopokea kiasi cha shilingi milioni  200 na kituo cha afya Igoma kilichopokea milioni 400 kutoka kwa serikali.


Awali uongozi wa Mkoa huo umetoa pongezi kwa jitahada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono ya kuleta maendeleo makubwa kwenye sekta ya afya hususani mkoa wa Mwanza ambao ni kitovu cha huduma na maendeleo ya kanda ya ziwa na nchi jirani.


MWISHO

Share To:

msumbanews

Post A Comment: