Mbunge wa Jimbo la Simanjiro aliyemaliza muda wake James Ole Millya akisalimiana na mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Bilionea Saniniu Kurian Laizer kwenye sherehe ya shukrani ya kupata madini ya Tanzanite ya thamani ya shilingi bilioni 7.7 kulia ni Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, (Marema) Justin Nyari na Diwani wa kata ya Naisinyai anayemaliza muda wake, Klempu Ole Kinoka.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, aliyemaliza muda wake James Ole Millya akizungumza kwenye sherehe ya mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Bilionea Saniniu Kurian Laizer ya kufanikiwa kupata madini yenye thamani ya shilingi bilioni 7.7 aliyofanya na wachimbaji wake 220.

MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, ambaye anamaliza muda wake, amesema kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanyika kwenye Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwenye Wilaya ya Simanjiro anatarajia atapita kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Octoba 25 mwaka huu.

Ole Millya aliyasema hayo jana kwenye sherehe ya kumshukuru Mungu na kuwapongeza wachimbaji wa madini ya Tanzanite iliyofanywa na mchimbaji maarufu Bilionea Saniniu Kurian Laizer.

Alisema ni maendeleo mengi yamefanywa na Rais Magufuli kwenye maeneo ya Simanjiro ikiwemo barabara ya lami kutoka Kia hadi mji mdogo wa Mirerani.

Alisema pia Rais Magufuli amefanikisha mradi mkubwa wa maji kutoka mto Ruvu hadi makao makuu wa wilaya hiyo mji mdogo wa Orkesumet ambao unaendelea kujengwa na kutarajiwa kukamilika mwaka huu.

Alisema pia mji mdogo wa Mirerani umetengewa mradi wa maji kutoka wilayani Arumeru mkoani Arusha unaoendelea kujengwa na kutarajiwa kukamilika mwaka huu.

"Kwa maendeleo haya aliyofanya Rais Magufuli sidhani kama kuna haja ya yeye kufanya kampeni zaidi ya kupita na mimi natarajia pia kupita kwa kishindo,״ alisema Ole Millya.

Alisema awali wakati ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ulipoagizwa kujengwa na Rais Magufuli, baadhi ya wananchi wa Mirerani walikuwa wanalalamika kuwa yeye amechangia kufanyika kwa hilo lakini sasa hivi wanajivunia.

״Kila mmoja hivi sasa anaona fahari ya kuwepo kwa ukuta huu ambao umesababisha madini ya Tanzanite yasitoroshwe nje ya nchi, yatambulike na kuthaminiwa na kunufaisha Taifa na kuzalisha mabilionea wapya kama kina Laizer," alisema Ole Millya.

Alisema wananchi wa eneo hilo wanatambua bajana msimamo wake thabiti wa kutokupokea rushwa kwani alikuwa anawatetea wachimbaji wadogo kwa muda wote wa ubunge wake hivyo anatarajia ataendelea na ubunge huo.

״Mimi japokuwa nimetokea kwenye familia duni lakini niliapa kuridhika na kile kidogo wananchi wa Simanjiro waliochonipatia bure kwa heshima kubwa hivyo nikaendelea kuwa nao bila kuchukua fedha chafu ambazo nilikuwa naambiwa nichukue ili nisiwatetee wachimbaji wadogo,״ alisema Ole Millya.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wa Mkoa wa Manyara, (Marema) Justin Nyari ambaye alikuwa mgeni rasmi wa sherehe hiyo alisema japokuwa hafanyi kampeni lakini Ole Millya anapaswa kuchaguliwa kuendelea kuongoza tena jimbo hilo.

Nyari alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa mnapokuwa na mbuge kama Ole Millya anayewatetea wachimbaji wadogo na wananchi kwa ujumla wanapaswa kumuunga mkono kwa kuendelea kuwa naye.

״Unapokuwa na mchezaji mzuri uwanjani kama Ole Millya mnatakiwa kuendelea kuwa naye na siyo kumbadilisha bila sababu yeyote hivyo tuendelee naye kwa kipindi kingine cha miaka mitano," alisema Nyari.
Share To:

Post A Comment: