.
Na WAMJW- DSM

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume ametoa wito kwa wananchi, hususan Jijini Dar es Salaam kutobwete na kuwataka kuendelea kuchukua hatua za tahadhari ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika kipindi hiki.

Dkt. Rashid Mfaume ametoa wito huo leo, wakati akipokea msaada wa barakoa 17,500 sawa na maboksi 350, na vipukusi (sanitizers) lita 700 ambayo ni sawa na madumu 140 yenye ujazo wa lita 5 kutoka kwa Shirika lisilo Lakiserikali la Medipeace linalohusika na mradi wa mama na mtoto katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Licha ya elimu tunayoendelea kutoa juu ya namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, tunawahamasisha wananchi wasibweteke katika kipindi hiki, ili kuumaliza kabisa ugonjwa huu katika nchi yetu, na hili linawezekana kabisa" alisema

Dkt. Rashid Mfaume aliendelea kusema kuwa, Msaada huo utaelekezwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya vya Sinza Hospitali, Vijibweni Hospitali, Rangi Tatu Hospitali, Kituo cha afya Kimara, Kituo cha afya Tandale, Kituo cha afya Mbezi, Kituo cha afya Round table, Kituo cha afya Kimbiji, Kituo cha afya Buguruni, Tegeta Dispensari, Bunju Dispensari.

Aidha, amefafanua kuwa, kumekuwa na ongezeko la wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya, hususan katika Jiji la Dar es Salaam baada ya Serikali kuziteua baadhi ya Hospitali kuwa vituo vya kutolea huduma za Corona, hivyo kuelekezwa msaada huo katika vituo vya Afya kutasaidia mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya Corona.

"Sasa hivi tumeona wagonjwa wameongezeka sana katika vituo vya kutolea huduma za Afya, mfano katika Mkoa wa Dar es Salaam baada ya Serikali kuitangaza Hospitali ya Amana kuwa kituo cha kuhudumia wagonjwa wa COVID-19, wagonjwa wengi wamekuwa wakienda katika vituo vingine, hivo msaada huu utasaidia sana kupambana dhidi ya maambukizi mapya" alisema.

Mbali na hayo, Dkt. Mfaume amewataka Wadau wengine kutoka Mashirika mbali mbali nchini kuendelea kuisaidia Serikali vifaa kinga vya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona ili kuvisaidia vituo vya kutolea huduma za Afya vyiweze kujitosheleza mahitaji hayo, hasa kutokana na vituo vya Afya kuwa sehemu inayopokea watu tofauti kwa wingi.

Hata hivyo, Dkt. Mfaume amewatoa wasi wasi Wananchi kuwa, hali ya Afya katika Mkoa wa Dar es Salaam ni shwari, huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua tahadhari za karibu dhidi ya maambukizi hayo ili kuumaliza kabisa ugonjwa huo nchini.

Nae, Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Medipeace Tanzania Bi. Sukyung Kim amesema kuwa, Medipeace inayofadhiliwa na KOICA imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika mkoa wa Dar-es-salaam.

Aliendelea kusema kuwa, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona, Shirika hilo linaunga mkono juhudi za Serikali za kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo kwa kutoa vifaa kinga ambavyo vitasaidia kwa Watoa huduma za Afya na wagonjwa wataofika kupata matibabu katika vituo hivyo.

Mwisho.
Share To:

Post A Comment: