Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema michezo ni afya, lakini pia michezo ni sehemu ya kujenga umoja, mshikamano na kuleta ari mpya katika kazi.
Profesa Mwakalila amesema hayo wakati akifungua bonanza la michezo kwa mwaka 2020 kwa Watumishi wa chuo hicho ambapo amesisitiza kuwa Michezo inaondoa misongo ya kazi, inaburudisha, na kuleta afya ya kimwili na kiroho.
“Michezo inaondoa tofauti na kuimarisha upendo mahali pa kazi,inaleta umoja na mshikamano, pia michezo ni dawa ya kulinda umoja mahali pa kazi, hivyo ninawaasa tuendelee kudumisha michezo ili tuendelee kuwa wamoja,”alisisitiza Prof. Mwakalila
Mkuu huyo wa chuo pia amewaahidi wanamichezo kuwa viwanja vyote vya michezo vilivyopo chuoni hapo vitaboreshwa ili viwe na hadhi ya kitaifa na kimataifa, huku akiwataka wanamichezo kuhakikisha wanafanya mazoezi ili kuwa na nguvu na uwezo wa kushiriki michezo kikamilifu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya michezo chuoni hapo Justine Kavindi ameshauri uongozi wa chuo kuhakikisha michezo inayofanyika katika kampasi ya kivukoni ifanyike katika kampasi ya karume Zanzibar kwa lengo la kuleta umoja na kuimarisha afya.
Kavindi Pia amemhakikishia Mkuu wa Chuo kuwa wanamichezo wote wataendelea kufanya juhudi ili kuhakikisha timu zote zinashinda katika mechizo mbalimbali na kuhakikisha Chuo kinaendela kuwa na sifa bora.
Michezo iliyoshiriki katika bonanza hilo ni pamoja na Mpira wa miguu, mpira wa pete, mchezo wa bao, mchezo drafti, karata, mchezo wa riadha, na kuvuta Kamba ambapo washindi katika timu zote hizo watazawadiwa zawadi mbalimbali ikiwemo mbuzi kwa mshindi wa kwanza katika kila timu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
10/1/2020
Post A Comment: