Serikali imeaandaa mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa Programu za Mafunzo Endelevu ya Walimu kazini ambazo zitakua na tija na pia kuongeza motisha kwa walimu.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini. 

Amesema  pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuboresha elimu kumekuwepo na changamoto hivyo mwongozo huo utasaidia kuondoa changamoto zinazojitokeza katika programu za mafunzo kazini kwa walimu ikiwemo kutokuwa na mwendelezo  na kukosekana kwa mfumo wa uratibu wa uendeshaji wa mafunzo.

Dkt. Akwilapo amewataka wajumbe wa mkutano kushiriki kikamilifu  kwa kutoa maoni ili kuandaa  miongozo ya utekelezaji wa Programu za Mafunzo Endelevu ya walimu kazini nchini. 

"Wizara ya Elimu imeona  ni muhimu kupata uzoefu kutoka kwa wadau na washirika wetu kutoka ndani na nje ya nchi kuhusu namna Programu za Mafunzo endelevu ya walimu kazini zinavyoendeshwa, naamini ushiriki wenu utasaidia kubaini maeneo muhimu katika kuratibu kazi zilizobaki," Amesema Dkt Akwilapo

Dk Akwilapo amesema kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikitekeleza programu za mafunzo kazi kwa walimu ikiwepo Mpango wa Tanzania UNESCO na UNICEF (MTUU)  na Programu ya Kutegemeza Elimu ya Msingi Kiwilaya (DBSPE) hivyo uwepo wa muongozo huo ni  muendelezo juhudi hizo katika kuhakikisha mafunzo kazini kwa walimu yanafanyika kwa ufanisi.

Nae Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema  wazo la kuwa na muongozo kuhusu mafunzo endelevu ya walimu kazini ni wazo ambalo nchi yoyote iliyo makini ambayo inayotaka kuwa na walimu bora katika elimu inapaswa kuzingatia kwani mafunzo ya awali ya walimu pasipo mafunzo endelevu kazini ni mafunzo yasiyo kuwa na tija na kwamba vitu hivi viwili vinategemeana.

" Katika kipindi hiki tumeamua kwa dhati kwamba baada ya mafunzo ya awali ya walimu watakapokwenda kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi huko wakute wabobezi ambao watawapokea na kuendeleza kuwapa utaalamu siku kwa siku ili waweze kukua na kuendelea kitaalamu," Amesema Dkt. Mutahabwa

Kwa upande wake Msahauri wa Elimu Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza (DFID)John Lusingu amesema uamuzi wa Serikali kuitisha kikao hicho cha wadau ni jambo jema kwa kuwa wadau wanapata nafasi ya kuchangia katika kuboresha badala ya mtu mmoja kuja na wazo na kutakiwa kufanyiwa kazi.

Mkutano wa wadau katika kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini  unafanyika kwa siku mbili  kuanzia Novemba 5, 2019 na unashirikisha wadau mbalimbali kutoka Idara ya Maendeleo ya Kimataifa DFID, Watafiti wa Elimu kutoka Marekani (RISE), EQUIP-T, Tusome Pamoja,  TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa wenyeji.
 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa kushirikishana uzoefu wa undeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini jijini Dodoma
Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamojana wadau wa elimu baada ya kufungua mkutano wa wadau wa kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: