Katika Picha ni kinu cha kuchakata zao la mpunga kinachotumiwa na wakulima wa umoja wa wakulima wa umwagiliaji Uliyanyama Wilayani Sikonge Mkoani Tabora, ili kuweza kuongeza thamani ya mazao yao.
 Bi Happiness Mpunda mkulima katika skimu ya kilimo cha Umwagiliaji Uliyanyama akiongea kuhusu faida alizozopata kutokana na kilimo cha Umwagiliaji.
Pichani ni ghala la kuhifadhia nafaka lililojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora.

Na Mwandishi wetu, Sikonge Tabora

UBORESHAJI wa miundombnu ya umwagiliaji katika Halmashauri ya Sikonge Mkoani Tabora umeongeza uzalishaji wa zao la mpunga, hivyo kuinua kipato cha wakulima wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari na Maafisa toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Katibu wa Chama Cha Wamwagiliaji cha Skimu ya Ulyanyama wilayani Sikonge Bw. Simon Kalosa amesema kuwa baada ya serkali kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na kutoa mafunzo ya uendeshaji na utunzaji wa skimu, uzalishaji wa mpunga umeongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.

Bw. Kalosa amesema kuwa wastani wa uzalishaji wa mpunga kwa sasa katika skimu ya Ulyanyama ni tani 8 kwa hecta wakati kabla ya uboreshaji wa miundombinu uzalishaji ulikuwa ni magunia sita hadi nane kwa ekari.

Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mpunga katika skimu ya ulyanyama Kalosa amesema hali za maisha ya wananchi wengi zimekuwa bora na wengi wameweza kujenga nyumba za kisasa na kusomesha watoto wao.

Kalosa amesema kuwa skimu ya ulyanyama ina jumla ya wakulima 306 ambao hujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na wengi wao wamefaidika na uwekezaji uliofanywa na serikali katika kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hiyo.

Akizungumza awali mkulima wa kilimo cha Umwagiliaji Bi. Happiness Mpunda amesema kilimo cha umwagiliaji kimebadilisha maisha yake na familia kwa ujumla kwani sasa anajitosheleza kwa chakula na kuinua kipato cha familia.

Bi.Mpunda amesema katika msimu wa 2018/2019 ameweza kuvuna magunia 35 kwa ekari ambapo kabla ya kupata mafunzo ya matunzo bora ya mashamba alikuwa akipata gunia sita tu kwa ekari.

” Kuna tofauti kubwa sana ya uzalishaji kabla na baada ya mafunzo ya uendelshaji na matunzo ya miundombinu ya umwagiliaji, tulipokuwa tunatumia mbinu za kienyeji tulitumia nguvu nyingi sana uzalishaji kidogo wakati kwa sasa ni kinyume chake”Alisema Bi. Mpunda.

Amesema kutokana na kilimo cha umwagiliaji ameweza kusomesha watoto watano na amenunua usafiri ambao umeweza kurahisisha mizungo ya kutafuta masoko ya mazao yake.

Naye mwenyekiti wa Chama Cha Wamwagiliaji cha Ulyanyama Bwn. Dikson Simbila amesema kuwa ijapokuwa masoko ya mpunga wanaolima lipo ndani nan je ya Halmashauri ya Sikonge bado bei ziko chini kinyume na matarajiao yao.

Bw. Simbila amesema ili kuongeza thamani ya mpunga wao, chama kilinunua kinu cha kukobolea mpunga ambao pia huweza kupanga madaraja mbalimbali ya mpunga tayari kwa kuuza. Kwenye masoko mbalimbali.

Amesema kutokana na bei kuwa chini inawalazimu kusubiri hadi mwezi Disemba ili walau wapate bei nzuri ya mpunga ambapo hii huchelewesha maandalizi ya mashamba kwa ajili ya msimu unaofuatia.

Akizungumza mapema, Mhandisi wa unwagiliaji wa mkoa wa Tabora Bwana Bahati Bulekele amesema kuwa a wake eneo linalofaa kwa umwagiliaji ni hecta 38,000 ambapo hekta 5,352 zimeshaendelezwa .

Mhandisi Bulekele amesema Mkoa wa Tabora una jumla ya skimu za umwagiliaji 58 katika halmashauri mbalimbali na kati ya hizo 16 ndio zinazofanya kazi kwa kiwango cha juu.

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ina mamlaka ya kuratibu, kuendeleza na kusimamia maendeleo ya sekta ya Umwagiliaji nchini ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali katika utekelezaji na kufanya mapitio ya sera ya Taifa ya umwagiliaji, mkakati wa maendeleo ya umwagiliaji.

Tume pia inaratibu shughuli zote za umwagiliaji katika sekta ya umwagiliaji zinazotekelezwa na wadau wengine wa maendeleo, kuuhamasisha na kudumisha ushirikiano na taasisi za kimataifa zenye kutekeleza majukumu yanayofanana na Tume.

Ends
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: