Na Mashaka Mhando, Moshi.
WANAHABARI kutoka vyombo mbalimbali katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, wamepigwa msasa kusaidia jamii katika masuala mbalimbali ya kisheria.
Mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Moshi yameandaliwa na Mfuko wa Legal Services Facility (LSF) yalilenga kuwajengea uwezo waandishi hao ili waweze kusaidia jamii katika majukumu yao.
Mmoja ya wawezeshaji kutoka katika Mfuko huo Jane Matinde, alisema mfuko huo ulioanzishwa mwaka 2011, lina lengo la kukuza upatikanaji Wa haki sawa kwa wote hasa wanawake kwa njia ya kisheria.
Alisema mfuko huo pia, hutoa fedha kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria ( Paralegal) Tanzania Bara na Visiwani.
Matinde alisema kukuza na kulinda haki za binadamu hasa kuwalenga wanawake masikini, wasichana na makundi mengine yanayoweza kudhuriwa kwa kuwapatia msaada wa kisheria.
"Tumelenga kuongeza ubora wa huduma za msaada wa kisheria na kujenga ufahamu wa haki za binadamu ili kujenga uwezeshaji wa kisheria katika wilaya zote zilizopo nchini," alisema Matinde.
Pia alisema kuwa wanalenga kutoa huduma hizo kwa watu binafsi na jumuiya mbalimbali zinasaidiwa kuhakikisha haki zao za kijamii na kiuchumi zinapatikana na malalamiko yao yanasikilizwa huku migogoro yao inatatuliwa na haki za msingi za binadamu zinalindwa.
Matinde alisema hivi sasa wamezifikia kata 1,750 hapa nchini ambako wanasaidia kutoa msaada wa kisheria katika matatizo mbalimbali baada ya kuwaelimisha na kuwapa mafunzo mbalimbali juu ya msaada wa kisheria.
Alisema kwa hapa nchini matatizo yanayoongoza kupatiwa msaada ni migogoro ya Ardhi, ndoa, mirathi, jinai, matunzo ya watoto na migogoro ya kazi kutoka kwa wafanyakazi.
Naye Veronica Ulomi alisema waandishi wa habari hao watashirikiana nao katika kuhakikisha wanaelimisha jamii juu ya namna ya kutafuta msaada wa kisheria katika vikundi mbalimbali vinavyotoa msaada wa kisheria vilipo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Victor Kisaka mwangalizi wa mkoa wa Tanga, alisema moja ya changamoto katika mkoa huo ni msaada wa kesi katika migogoro ya ardhi hasa kutokana na kuwepo kwa mashamba makubwa ya mkonge.
Mmoja ya wawezeshaji katika semina hiyo ya siku moja Nevile Meena kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF), alisema waandishi wa habari wafanyie tafiti habari zao kabla ya kuzichapisha ili kuepuka migogoro inayojitokeza katika jamii ikiwemo serikali.
Alisema mwandishi bora ni yule anayefanya kazi za uchunguzi na kutafuta ukweli wa jambo kwa kuwapa nafasi watu wengi zaidi katika habari yake ili kuondoa uwezekano wa kuandika habari za uongo.
Post A Comment: