Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na Mathias Canal
Katika
swala la kujifunza katika jamii yetu bado limekuwa ni gumu sana.
Ukikutana na watu kumi ukiwauliza unapenda kusoma vitabu utasikia
wakisema napenda kusoma vitabu ila sina muda. Muda umekuwa kisingizio
kwa watu wengi kutupia lawama zao zote katika muda. Watu wanasingizia
muda umekuwa tatizo lakini mimi nakataa nasema muda sio tatizo. Habari
njema ni kwamba Mungu ametuzawadia zawadi au rasilimali muhimu kuliko
zote ambayo ni muda. Kila binadamu aliye hai ana muda wa masaa 24 kwa
siku hivyo kwa wiki moja kila mtu ana jumla ya masaa 168 sasa katika
masaa 168 kwa wiki nzima unakosa muda kweli wakusoma vitabu na kuongeza
maarifa?
Ni
hivi karibuni tu wakati wa ziara ya Kikazi katika Wilaya ya Itilima
vilevile Wilaya ya Bariadi, Waziri wa Kilimo alizuru kwa ajili ya
kufuatilia mwenendo wa biashara ya Pamba ili kumulika madhila wanayopata
wananchi kwa kucheleweshewa fedha kutokana na sintofahamu ya wanunuzi
kujitokeza kwa wingi katika ununuzi pamoja na wakulima kuwa tayari
wamekusanya Pamba kupitia vyama vyao vya Ushirika. Hapa Mhe Japhet
Hasunga anakutana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka huku akiwa
na vitabu zaidi ya 100 ofisini kwake alivyokwishavisoma katika kipindi
cha mwaka mmoja.
Kama
mchambuzi na mdadisi wa mambo nilifanya mazungumzo ya takribani dakika
15 hivi kubaini dhana ya kusoma vitabu, Uongozi na Uwajibikaji. Rc Mtaka
anasema “Comrade Mathias akili yako inahitaji maarifa kila siku ili
iweze kukua, akili yako inahitaji chakula kila siku kama unavyolisha
tumbo lako nalo linahitaji maarifa. Hazina ya akili yako ni maarifa na
maarifa yanapatikana katika kusoma vitabu, makala chanya, na siyo kusoma
magazeti ya udaku, kusikiliza habari nyepesi nyepesi zisizokuwa na
upembuzi yakinifu.
Jinsi
unavyokaa bila kusoma ndivyo akili yako inakaa inazidi kulala ukisoma
nayo inazidi kuamka. Jitahidi kusoma na kufikiri kila siku ndio zoezi la
akili yako. Kuwa na shahada, astashahada, stashahada, uzamili na
uzamivu siyo mwisho wa kusoma au kujifunza bali huo ndio mwanzo wa
kujifunza. Usiridhike na maarifa uliyonayo bali kuwa na njaa kali ya
maarifa elimu uliyopata darasani ni msingi tu wa kusoma. Mtu anayesoma
anakuwa tofauti sana na mtu asiyesoma vitabu tafadhali nakuomba anza
kujifunza kuna faida nyingi zisizoelezeka.
Kusoma
vitabu sio jambo la lelemama ni jambo la kufanya maamuzi na kutenga
muda maalumu kwa ajili hiyo, Lengo kubwa linalowafanya waandishi wa
vitabu kuandika vitabu ni kuweka maarifa yao kwenye maandishi, Kwa
hakika vitabu huongeza sana uwezo wa kufikiri. Unaposoma vitabu
unafahamu mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi; mara nyingine kitabu
kitakuacha na maswali ambayo yatakufanya utafakari kwa kina zaidi juu ya
mambo mbalimbali.
Rc
Mtaka ni kijana kabisa kiumri ambaye hajavuka hata miaka 40 bila shaka.
Anaeleza Maisha yana changamoto mbalimbali; hivyo utahitaji kitu cha
kukuhamasisha kutoka hatua moja hadi nyingine. Kwa kusoma vitabu vya
hamasa kuhusu maswala mbalimbali ya maisha utaweza kuhamasika zaidi.
Unapotumia
muda wako kusoma vitabu, ni wazi kuwa hutopata muda wa kupoteza, Kusoma
vitabu kutakufanya utumie muda wako kuongeza maarifa yako zaidi.
Tofauti kubwa iliyopo kati ya kusoma vitabu na kuangalia televisheni ni
juu ya kuongeza ubunifu wako. Kusoma vitabu hukufanya uondoke katika
lindi kubwa la mawazo yanayokutesa na kukutafakarisha juu ya mambo
mengine. Waandishi wa vitabu hujenga mazingira ambayo msomaji hujihisi
yumo ndani yake.
Dakika
mazungumzo yangu na Rc Mtaka ananikumbusha kuwa “Mathias Kadri
unavyosoma vitabu vingi kutoka kwa waandishi mbalimbali, ndivyo
unavyojitajirisha juu ya misamiati. Kuwa na ukwasi wa misamiati husaidia
sana katika maisha ya kila siku. Huongeza kujiamini na uwezo wa
kuzungumza mbele ya hadhira. Hadhira yoyote huvutiwa zaidi na
mzungumzaji mwenye kujiamini na mwenye uwezo wa kucheza na misamiati ya
lugha kwa umaridadi kadri ya muktadha.
Katika
ziara hiyo niliondoka Mkoani Simiyu nikiwa na kumbukumbu nzuri na
umuhimu wa kukutana na Rc Antony Mtaka nimeamini katika kusoma vitabu
Unapata kujua mambo mapya, Ukuaji binafsi wa weledi, kuongeza uelewa, na
Kukupa msukumo wa kufanya Maandalizi kabla ya jambo lolote.
Naamini
sasa pamoja na mawazo chanya ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe antony Mtaka
unakubaliana na mimi kuwa kuna vito vya thamani sana vilivyofichwa
kwenye vitabu ambayo watu wengi hawavifahamu.
Ni
muhimu ukajijengea utamaduni wa kusoma vitabu mara kwa mara kadri
uwezavyo. Unaweza kutumia programu kama vile Balabolka ili kubadili
vitabu kuwa sauti na uvisikilize badala ya kuvisoma.
Post A Comment: