KUFUATIA picha zilizosambaa mitandaoni zikimuonyesha Mbunge wa Ulanga, Morogoro (CCM), Goodluck Mlinga, kuonekana ameshika sindano kama anamchoma mwanafunzi chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi, jambo hilo limeibua hisia tofauti miongoni mwa wadau huku wakihoji kuhusu mtu asiye na taaluma ya afya anapata wapi mamlaka ya kutoa chanjo hiyo.

“Siasa imeingia sehemu mbaya sana, tiba si eneo la mzaha kiasi hiki, hili ni eneo hatari, na mchezo huu kwa afya za watu unaweza kusababisha maumivu hata ulemavu, si kila mtu anaweza kutoa chanjo,” alitoa maoni mmoja wa wadau kupitia mtanda wa Twitter.

Akijibu hoja hiyo kupitia akaunti ya Twitter, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema jambo hilo si sahihi kwani wanaotakiwa kutoa huduma za afya ni watu wataalamu wa tiba na si mtu mwingine huku akimuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo kutoa maelekezo kwa waganga.

“Hii si sahihi, tayari nimeshamuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kutoa maelekezo mara moja kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya kusisitiza uzingatiwaji wa Miongozo ya Utoaji wa Huduma za Afya nchini, masuala ya kitaalamu yafanywe na wataalamu,” alisema Ummy.

Kitendo alichokifanya Mlinga kimeelezewa na baadhi ya watu kama kufanya mambo ya afya yawe ya  kisiasa japo haijulikani kama mbunge huyo alikuwa akimchoma kweli mwanafunzi huyo au alishika tu sindano mabegani mwake kama ishara ya uzinduzi wa chanjo na kuhimiza wanafunzi wajitokeze kupata kinga hiyo.

Hivi karibuni, Wizara ya Afya ilizindua chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wa umri wa miaka 14 ili kuwakinga na matatizo hayo ambayo hupoteza idadi kubwa ya akina mama.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: