Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewatoa wasiwasi wapenda soka nchini wote ambao wamepanga kuenda kuutazama mtanange wa aina yake kati ya Yanga dhidi ya Simba katika dimba la Taifa Aprili 29, 2018 kuwa hali ya usalama imeimarishwa kila idara.

Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na uongozi wa TFF, alasiri ya leo zikiwa zimebakia takribani siku 5 kuelekea mchezo huo na kusema watashirikiana na Jeshi la Polisi katika kulinda hali ya usalama ndani ya mchezo huo pamoja na wananchi watakao kuwa wanatazama mechi.

"Mageti yanatarajia kufunguliwa mapema kuanzia saa 2 asubuhi ambapo vyakula na vinywaji vitapatikana ndani. Vile vile Jeshi la Polisi limetuhakikishia kuwa ulinzi utakua wa hali ya juu na kuwatahadharisha wale wote wenye nia ya kufanya vitendo vya uovu kuacha mara moja",imesema taarifa hiyo.

Pamoja na hayo, taarifa hiyo imeendelea kwa kusema "mamlaka ya uwanja imethibitisha kuongezeka kwa kamera za uwanjani ambapo sasa zimefikia 109 ambazo zitakuwa zinafuatilia matukio yote".

Kwa upande mwingine, TFF imesema zoezi la kununua tiketi za kuenda kutazama mubashara mtanange huo limeshaanza kupitia katika mitandao mbalimbali ya simu kama ilivyokuwa awali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: