TFF imetangaza mchezo wa fainali ya Azam Sports Federation Cup itachezwa Juni 2, 2018 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.
Mwaka 2017 mchezo wa fainali wa kombe hilo ulichezwa uwanja wa Jamhuri Dodoma na kuishuhudia Simba ikitwaa taji hilo mbele ya Mbao baada ya ushindi wa magoli 2-1.
Mapema kabla ya michezo ya kombe hilo kuanza, TFF kupitia kwa afisa habari wake Alfred Lucas ilitangaza kwamba fainali ya mwaka huu itachezwa Dar lakini baadaye imetangazwa kuchezwa Arusha.
Afisa masoko wa TFF Aron Nyanda ametaja baadhi ya sababu za kuupeleka mchezo huo mkoani Arusha.
“Tangu Rais wa TFF anaingia madarakani alielezea vitu vingi sana na alisema, kutakuwa na na usawa katika kuendesha mpira wa Tanzania na ukiangalia fainali za FA Cup zimekuwa zikizunguka ilichezwa Dodoma na sasa Arusha.”
“Kuna sehemu nyingine hawajaona ligi kuu kwa muda mrefu, tukiwapelekea mashindano makubwa ni hamasa pia kwa mkoa na nchi kuona kwamba mpira unazunguka nchi nzima na kila mtanzania anapata fursa ya kuona mashindano nchini kwake.”
“Tumeichagua Arusha kwa kuangalia vigezo vya uwanja ambavyo vinatumika, uwanja wa Sheikh Amri Abeid ni uwanja mkubwa kwa hiyo kuwepo pale kutakuwa na hamasa kubwa na watu watakuwa wengi sana.”
Tayari Mtibwa Sugar imeshafuzu kucheza fainali ya ASFC mwaka 2018 baada ya kuifunga Stand United 2-0 katika mchezo wa nusu fainali, Mtibwa inasubiri mshindi wa mechi kati ya Singida United na JKT Tanzania.
Post A Comment: