Nyota wanne kutoka timu tofauti zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, wameingia kwenye rada za Simba na huenda wakasajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.
Nyota hao ni Ditram Nchimbi wa Njombe Mji, Abdallah Mfuko (Mwadui FC), Idd Kipagwile (Azam) na Habib Kyombo (Mbao FC).
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu amevutiwa na wachezaji wengi wakiwemo hao.
Manara alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa, kutokana na kikosi chao kwa msimu huu kuwa bora, hawatarajii kukifanyia marekebisho makubwa katika kipindi kijacho cha usajili wa dirisha kubwa.
“Kwa sasa ni mapema mno kusema nani na nani amenivutia lakini wapo walionivutia mpaka sasa.
“Kuna straika mmoja namba tisa wa Njombe Mji mrefu hivi (Ditram Nchimbi) yule ni mchezaji wa aina ya John Bocco, pia yupo Idd Kipagwile wa Azam FC, ile ni mashine nyingine.
“Pia Habib Kyombo ana ‘footwork’ nzuri, lakini pia yupo beki mmoja hivi wa kati anacheza Mwadui (Abdallah Mfuko), hao ndiyo wamenivutia ingawa siwezi kusema moja kwa moja tutawasajili.
“Kwa sasa tunaangalia namna ambavyo tutachukua ubingwa wa ligi na nadhani tukishachukua hatutabadilisha kikosi chetu kwa kiasi kikubwa, lakini katika marekebisho hayo tutafuata ripoti ya mwalimu anataka nini ingawa sisi kama viongozi tunaona sehemu ambazo zina upungufu,” alisema Manara.
Post A Comment: