Hali ni shwari mkoani Manyara. Hakuna dalili za maandamano. Hata hivyo askari polisi wakiwa na magari, pikipiki na kutembelea kwa miguu walionekana wakizunguka sehemu mbalimbali ili kuimarisha ulinzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP) Agustino Senga akizungumza  kwa njia ya simu  leo Aprili 26, amesema mkoa huo upo shwari kabisa. 
 
Kamanda Senga amesema polisi wapo kwenye maeneo tofauti ya mkoa huo wakiendelea na kazi ya ulinzi wa raia na mali zao.

"Kwenye mkoa wangu hakuna mtu aliyeandamana wala aliyehamasisha mtu kuandamana wala hakuna aliyekamatwa juu ya hilo kwa kuhamasisha wala kuandamana," amesema kamanda Senga.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zephania Chaula akizungumza juu ya maandamano hayo, aliwataka wananchi wenye nia hiyo kufanya shughuli zao za maendeleo na kuachana na suala hilo.

"Kama kuna mtu ana hoja yoyote aje mezani tuzungumze juu ya hoja yake na siyo kutuletea habari za mambo ya kuandamana ambayo hayana tija yoyote kwa jamii," amesema Mhandisi Chaula.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: