Katika kuonesha kwamba wanaisimamia Serikali ya awamu ya tano kwa ukamilifu, Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Ubungo umefanya ziara katika shule ya Sekondari ya Matosa iliyopo wilayani humo ili kujionea utekelezaji wa ilani ya chama hicho katika sekta ta elimu.

Ziara hiyo ambayo ilidumu shuleni hapo takribani masaa mawili ililenga kukagua maendeleo ya shule hiyo, kujionea changamoto ya vyoo, kuzungumza na wanafunzi, waalimu lakini pia wakitumia fursa hiyo kugawa zawadi ya madaftari zaidi ya mia nne kwa wanafunzi waliofanya vizuri pamoja na wale wanaotoka katika madarasa ya mitihani (kidato cha pili na nne).

Akizungumza na wanafunzi hao, Katibu wa UVCCM wilaya ya Ubungo, Lea Mbeke ambaye alikua kiongozi wa msafara aliwataka wanafunzi hao kuzingatia elimu, kuwa na nidhamu pamoja na kuutunza uzalendo wa Nchi ambao Rais John Magufuli amekuwa akiuimiza kwa wananchi wote.

Lea alisema wao kama vijana wameamua kuonesha kwa vitendo namna gani wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kuleta elimu bure kwa kila mtanzania ambapo kwa kuanzia wametoa idadi ya madaftari 400 katika shule hioyo.

" Sisi kama vijana hatupaswi kuiachia serikali kila kitu ikafanya, lazima tuunge juhudi za Rais kwa vitendo, hivyo niwaombe sana msome kwa bidii na pale mnapokua na tatizo au changamoto yoyote msisite kuwasiliana na mimi ili tuangalie namna gani ya kuweza kuzitatua," amesema Lea.

Amesema Sekondari ya Matosa imekuwa ya kwanza kunufaika na ziara hiyo huku akiweka wazi mpango wake wa kuzitemebelea shule 28 za sekondari zilizopo wilayani hapo na zile za binafsi na baada ya hapo watazitembelea shule za msingi.

" Serikali imeamua kutoa elimu bure ili kila mtanzania asome hivyo hakikisheni mnasoma kweli kweli, hatukuja kisiasa hapa tumekuja kujionea changamoto zenu na kuangalia namna gani tunaweza kuzitatua na kusaidiana kama vijana, huu ni mwanzo tu tutawatembelea kadri tutakayojaliwa," alisema Seif Kimbangu ambaye ni Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Mkoa.

Nae Vaileth Soka ambaye ni Mwenyekiti wa Kata ya Mabibo wa chama hicho aliwataka wanafunzi hao kuzingatia usafi, nidhamu pamoja na kusoma kwa bidii ili kuja kuwa viongozi wakubwa wa baadae, na kuweza kusaidia familia na Nchi kutokana na elimu waliyoipata.

Kwa upande wake Kiongozi wa wanafunzi, Shani Hashim aliwashukuru viongozi hao kwa kuwatembelea na kujionea changamoto zinazowakabili na kuwashukuru kwa zawadi ambazo wamewaletea.

" Ni jambo la faraja kupata ugeni mkubwa shuleni kwetu zawadi hizi mlizotupatia zikawe chachu ya sisi kuweza kufanya vizuri zaidi, tunamshukuru Rais kwa elimu bure na tunampenda sana tunaomba na wadau wengine waweze kuisaidia elimu yetu," amesema Lea.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: