KAMPUNI ya Katani Limited yenye makao makuu yake jijini Tanga, imesema kadiri itakavyokuwa na uzalishaji wa kiwango cha juu, itaidhamini moja kwa moja Klabu ya Coastal Union inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, kutangaza kuingia udhamini wa mashindano ya ‘Tanga City II Marathon 2018’, mkurugenzi wa kampuni hiyo, Juma Shamte, alisema kuwa wamejiingiza kwenye michezo kama njia mojawapo ya kuhamasisha ulimaji wa zao la mkonge.

Alisema kadiri watakavyoweza kukua na kuzalisha kwa wingi bidhaa zitokanazo na mkonge, wataweza kuwa na fursa zaidi ya kujiingiza katika michezo na kwamba wanaweza kukutana na viongozi wa Coastal wakatazama kama wanaweza na wao kuifadhili.

“Kadiri tunavyokua na kuzalisha tutaweza kutoa fursa zaidi za kujiingiza katika michezo, ni suala la kufanyia kazi kama tunaweza kukutana na viongozi wa Coastal na sisi tukaona tunashiriki vipi. Ni jambo la kukaa pamoja nao,” alisema Shamte.

Shamte alisema kampuni hiyo ambayo ina mashindano yake ya kila mwaka ya ‘Mkonge Cup’, inashiriki kusaidia timu mbalimbali za madaraja ya chini, kudhamini mashindano ya baiskeli, mpira wa pete pamoja na riadha.

Kampuni hiyo imekabidhi hundi ya shilingi milioni 7 kwa waandaaji wa mashindano hayo ambayo yatafanyika Machi 31 na jumla ya washiriki 500 hadi sasa wamejiandikisha kushiriki mbio hizo.

Mratibu wa mashindano hayo Juma Mwajasho alisema kwamba mbio ndefu zitakuwa za kilomita 21 na 10 pamoja na mbio fupi za kilomita 5 ambazo mara nyingi ni za watu wa aina mbalimbali kukimbia kama kujifurahisha.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: