WafanyaBiashara Mkoani Rukwa wamemuomba Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kuamua hatima ya pombe yao aina ya ‘viroba’ kwani wamevifungia stoo huku  wakidaiwa mikopo na kodi ya pango katika maeneo waliyovihifadhi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani hapa, Sadrick Malila, ndiye aliyetoa ombo hilo wakati akitoa taarifa ya hali ya biashara mkoani wakati wa kikao cha baraza la mkoa.

Alisema serikali ilipiga marufuku biashara hiyo kwa maelezo kuwa viroba vinachafua mazingira na wafanyabiashara walishavinunua ikiwa ni biashara halali, lakini serikali imekuwa kimya na hawajui hatima yake. Huku wakiwa wamechukua mikopo katika mabenki na taasisi nyingine za kifedha na wanaendelea kudaiwa mikopo hiyo na riba, kitendo kinachowafanya wazidi kuwa maskini na hawajui serikali inafikiria nini kuhusu suala hilo.

‘’Tunajua mwenyekiti hili suala liko nje ya uwezo wako, lakini una nafasi ya kuwasiliana na waziri mwenye dhamana ili aone atatusaidiaje wafanyabiashara, mitaji yetu imekwama kwenye viroba, serikali iko kimya na tunaendelea kudaiwa kwa kuwa fedha tulikopa benki, aone namna ya kutusaidia kwani suala hili inazidi kututia umaskini,’’ alisema Malila.

Alisema serikali inawahimiza wawekezaji katika viwanda,  lakini  wafanyabiashara wanaogopa kuchukua mikopo ili wapate mitaji kutokana na riba kubwa zinazotozwa na mabenki licha ya  Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupunguza  riba kwa mabenki hayo  kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12.  
Share To:

Post A Comment: