Bodaboda afariki kwa kucharangwa mapanga
DEREVA wa bodaboda, Amani Mkumbo (45), mkazi wa mtaa wa Mabambasi, Kata ya Ndembezi mjini Shinyanga, ameuawa na watu wasiojulikana.


Baada ya kuuawa, watu hao walimnyang’anya pikipiki yake  iliyokuwa na namba za usajili MC 883 BSL na kisha kuondoka nayo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD)  Shinyanga, Claud Kanyorota, alithibitisha  kutokea kwa tukio hilo ambalo limetokea juzi saa   5.45 usiku  katika kijiji cha Imalilo, kata ya Kitangili mjini humo, ambako alikuwa amewapeleka wateja wake.

Kanyorota alisema dereva huyo aliuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani  na kumcharanga kwa panga maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Alisema dereva huyo alifanyiwa unyama huo na  abiria alikuwa amewapakia maarufu kama mshikaki na alifariki wakati akipelekwa kwenye matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga.

“Ninachowaomba madereva wa bodaboda wachukue elimu waliyopewa na Jeshi la Polisi, waache kufanya kazi nyakati za usiku," alisema Kanyorota.

Naye Ramadhani Shija, mwendesha bodaboda alisema wimbi la mauaji na kutekwa madereva limeanza kuibuka tena kwa sababu awali lilishamiri na Jeshi la Polisi  lilifanikiwa kulimaliza.

Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Shinyanga, Wenceslaus Modest, alisema Mkumbo hakuwa mwanachama wao, lakini madereva wote waendesha  bodaboda walikwisha pewa elimu ya kujilinda na kutoendesha  pikipiki nyakati za usiku.

Mke wa marehemu, Josephine  Kitundu, alipohojiwa alidai kuwa mume wake alikuwa na kawaida ya kurudi usiku katika kazi yake hiyo lakini juzi kabla ya tukio hilo,  aliondoka kwenda kwenye kazi yake akiwa salama.

Alisema alishangaa kuona majira ya saa sita usiku  baadhi ya askari wakimfuata nyumbani kwake akiwa amelala bila kumwambia chochote na kutaka aende  akatoe maelezo kituo cha polisi  dhidi ya mume wake.

“Nilikuwa nimelala nikasikia napigiwa hodi majira ya saa sita usiku. Nilipofungua  mlango walikuwa askari walionifuata na kunieleza niondoke nao mpaka kituoni bila  kunieleza chochote.

Nilipofika  waliniambia nitoe maelezo ya mume wangu  ila hawakuniambia kama amefariki dunia, walichonieleza niwahi alfajiri Hospitali ya Rufani kumbe alikuwa amekwishafariki,” alisema
Share To:

msumbanews

Post A Comment: