IMEBAINIKA baada ya serikali kuzuia utengenezaji na uuzaji wa pombe kali zilizofungwa kwenye vifungashio vya plastiki maarufu kwa jina la ‘viroba’, kumeibuka wimbi la pombe zingine zilizopo kwenye chupa ambazo zinauzwa kwa bei ndogo.

Zuio hilo la serikali lilitolewa Februari 16, mwaka jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwa katika ziara mkoani Manyara ambapo alisema utekelezaji wake ulianza Machi Mosi mwaka jana, ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa kwa kuwa viroba vilikuwa vinabebeka kwa urahisi.

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari  mkoani Dodoma, umebaini pombe hizo ndizo  hivi karibuni zililalamikiwa na baadhi ya wafanyabiashara  kuwa zimekuwa zikikwepa kodi kutokana na kutofautiana kwenye uuzaji.

Katika uchunguzi huo, waandishi walishuhudia aina tofauti zaidi ya 20 huku nyingi zikitofautiana kwa bei licha ya kuwa ni aina moja na ujazo sawa za zingine zikitumia ‘brand’ ya watu wengine.
Pombe hizo zipo kwenye vichupa vidogo ambavyo nembo zinazoonyeshwa kutengenezwa Dar es Salaam na Mwanza na zingine kutoka Arusha, Shinyanga, Kilimanjaro na Geita.

Kadhalika, pombe hizo baadhi zinaonekana hazina stika za utambulisho zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA), zingine zina nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), lakini hazina stika ya TRA, pia zingine hazina stika za Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) na nyingine hazina stika yoyote. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: