Pamoja na uongozi wa Simba kutoweka bayana muda wa mkataba wa kocha wake mpya Pierre Lechantre kuitumikia timu hiyo, takwimu zinaonyesha Mfaransa huyo hajawahi kukaa katika klabu moja zaidi ya mwaka.
Uongozi wa Simba umemtangaza Mfaransa Lechantre kuwa kocha mpya wa klabu hiyo akichukua mikoba ya Mcameroon Joseph Omog aliyetimuliwa hivi karibuni
Ujio wa kocha huyo Mfaransa unaifanya Simba kuwa imefundishwa na makocha tisa tangu ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2011-12 ikiwa chini ya Mserbia, Milovan Cirkovic.

Kwa mujibu wa mtandao wa http://www-herzog.transfermarkt.kr unajihusisha na kutoa takwimu za masuala mbalimbali ya michezo umeonyesha kocha Lechantre anawastani wakufundisha timu si chini ya mwaka kabla ya kuondoka.

Mfaransa huyo aliwashangaza watu pale alipoamua kuvunja mkataba wake wa kuifundisha Senegal wiki mbili baada ya kukubali kuchukua jukumu hilo mwaka 2012.
Lechantre aliimbia Senegal press agency (APS)“Nilipata mkataba wiki iliyopita, lakini hiyo siyo kigezo pekee cha mimi kuendelea na jukumu langu la kuiongoza timu ya Senegal kama wameshindwa kunitimizia matakwa yangu.”

Viongozi wa Senegal walishindwa kumlipa mshahara wake wa miezi sita aliyotaka kulipwa kwanza kabla ya kuanza kazi.

Mfaransa huyo alianza kufundisha Afrika na timu ya taifa ya Cameroon kuanzia (Jan 1, 1999) hadi (Jun 30, 2001) sawa na siku (911).

Baada ya hapo akatimkika Qatar akaifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo kuanzia Agosti 1, 2001     hadi Desemba 31, 2001,sawa na siku 152.

Akajiunga kuifundisha klabu ya  Al Ahli ya Qatar alidumua nayo kwa siku 123 tu kuanzia Julai 1, 2003 hadi Novemba 1, 2003, kabla ya kutimkia timu nyingine ya Al Sailiya ya Qatar aliyokaa kwa siku 242 kuanzia Novemba 1, 2003, hadi Juni 30,2004.
Lechantre alirejea Afrika baada ya kupata mkataba wa kuifundisha Mali kwa muda mfupi kwa lengo la kuwapa tiketi ya Kombe la Dunia 2006, alifundisha hapo kwa siku 240 kuanzia Machi 5, 2005 hadi Oktoba 31, 2005.

Baada ya kushindwa kuipeleka Mali katika Kombe la Dunia 2006, Lechantre alitimkia katika klabu ya Al Rayyan ya Qatar akifundisha kwa siku 276, kuanzia Oktoba 1, 2006 hadi Julai 4, 2007.

Kuanzia Julai 4, 2007 hadi Desemba 31, 2007 alibukia Morocco na kujiunga na klabu ya MAS Fes aliyodumu nayo kwa siku 180 tu.

Club Africain ya Tunisia ilimchukua Mfaransa huyo  kuanzia Juni 12, 2009 hadi Aprili 8, 2010. Ndiyo klabu aliyokaa kwa muda mrefu zaidi alidumu kwa siku 300, baada ya kuiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya pili na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mafanikio aliyoyapata Club Africain yalivutia miamba mingine ya Tunisia, CS Sfaxien aliyokaa kwa siku 166 kuanzia Juni 22, 2010 hadi Desemba 5, 2010 kabla ya kutupiwa virago.

Baada ya kuchemsha Tunisia akatimkia Qatar na kujiunga na klabu ya Al Gharafa aliyokaa kwa siku 196, kuanzia Machi 19, 2012 hadi Oktoba 1, 2012.

Kocha Lechantre aliweka rekodi ya kufundisha siku 39, katika klabu ya Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi 19, 2012 hadi Aprili 27, 2012. Baada ya kuondoka Qatar aliibukia Libya na kujiunga na klabu ya Al-Ittihad aliyokaa kwa siku 187,kuanzia Machi 30, 2015 hadi Oktoba 3, 2015.

Kocha huyo mwenye bahati ya kufundisha mataifa ya Afrika, alipata ulaji Januari 13, 2016 wa kuifundisha Congo Brazzaville, lakini mkataba huo ulivunjwa ikiwa bado una miezi 17 mbele.

Novemba 15,2016, Congo ilitangaza kuvunja mkataba wake na kocha Lechantre baada ya kufungwa na Uganda 1-0 na kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018.
Ni kama mkataba wa Simba na kocha huyo utakuwa kipimo kwa pande zote mbili kwani timu hiyo pia imekuwa na historia ya kutodumu na makocha hasa pale mambo yanavyowaendea kombo.

Hivi karibuni Simba ilivunja mkataba wa kocha Joseph Omog na kuifanya iweke rekodi ya kufundishwa na makocha nane ndani ya kipindi cha miaka tisa ambao ni Patrick Liewig, Abdallah Kibaden, Zdravko Logalusic, Patrick Phiri, Goran Kopunovic, Dylan Kerr, Jackson Mayanja na Omog.

Hata hivyo wakati wengi wakidhani kibarua cha Masoud Djuma kinaweza kuota nyasi kutokana na ujio wa Lechantre, kocha huyo ameahidi kuendelea kuendelea kufanya kazi na raia huyo wa Burundi kama sehemu ya benchi lake la ufundi.

"Nimefurahi kuona timu ikicheza vizuri na kupata matokeo yanayofurahisha. Nampongeza kocha aliyepo kwa kile anachokifanya ndani ya timu. Naomba watu wasahau kuhusu rekodi yangu ya huko nyuma na kutazama zaidi kile nitakachokifanya ndani ya klabu hii.

Nimekuja kwa jukumu la kuhakikisha Simba inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ambalo sio jepesi. Naahidi kushirikiana vizuri na benchi langu la ufundi ili tufanikishe hilo. kuhusu mbinu ya ufundishaji nadhani ninapendelea zaidi mfumo huu wa 3-5-2 ambao Simba waliucheza juzi kwa sababu napenda soka la kushambulia na kuvutia," alisema Lechantre.

Kocha Masoud Djuma alisema hana tatizo na ujio wa Kocha Lechantre na yuko tayari kushirikiana naye ili kupeleka mbele gurudumu la Simba.

"Binafsi sina kinyongo na kocha anayekuja na nitafanya naye kazi bila tatizo lolote. Nitaandaa ripoti na kuikabidhi kwake na kile atakachokiamua baada ya kuipitia ripoti nitalazimika kukifuata.

Kama akiona tuendelee na hiki nilichokianza nitatii maagizo yake lakini kama akiamua kuleta mabadiliko, nitalazimika kukubaliana nayo kwa sababu yeye ndio bosi," alisema Djuma.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: