Magari zaidi 200 yakiwepo ya watalii yaliyokuwa yanaelekea Karatu kwenda Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti yamekwama katika eneo la Makuyuni baada ya daraja kusombwa na maji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Kamanda ya Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amesema jitihada za kutengenezwa njia ya muda zinaendelea.
Amesema daraja hilo limesombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Wilaya ya Monduli.
"Hadi sasa hakuna vifo ambavyo vimetokea ila ni kusombwa kwa daraja ambalo lilikuwa linaendelea kujengwa," amesema.
Baadhi ya madereva waliokwama Ismail Kessy na John Michael wamesema tangu saa 12 alfajiri wamekwama katika eneo hilo.
"Hii si mara ya kwanza daraja hili kusombwa na mafuriko tunaomba Serikali kuingilia kati kwani tuna watalii ambao walipaswa kuwa Serengeti lakini wamechelewa," amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii (TTGA), Khalifa Msangi ameomba daraja hilo kujengwa kwa ubora unaostahili ili kuondoa adha ya kuharibiwa na mafuriko mara kwa mara.
Post A Comment: