Kama ulikuwa unaudhika kila ukiona askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, angalau sasa unaweza kuwa na ujasiri wa kukabiliana nao kisheria.

Ni kwa kutumia elimu iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambaye jana alitoa ufafanuzi wa jinsi askari hao, maarufu kwa jina la Trafiki, wanavyotakiwa kufanya kazi.

Amezungumzia jinsi trafiki anavyotakiwa kufanya iwapo atasimamisha gari yako, makosa anayotakiwa kuyahoji na hatimaye kukutoza faini kulingana na wakati na hata utendaji wa polisi wanaozunguka na pikipiki, maarufu kwa jina la tigo.

Na faraja zaidi ni kauli yake kwamba si kila kosa linastahili faini na kuwataka trafiki kuwa makini ili kuondoa malalamiko ya uonevu na kuwakandamiza raia.

Mambosasa alitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM na baadaye kuzungumza na Mwananchi kufafanua maelezo yake.

Alishangazwa na askari wanaokamata gari mchana kwa kosa la kutowaka taa na kutoza faini.

Alitaja makosa mengine kuwa ni askari kukamata gari bila kujua kosa la msingi na kulazimika kuanza kulikagua kwa lengo la kubaini kosa.

Pia alieleza kwamba askari wanaotumia pikipiki maarufu kama ‘tigo’, hawaruhusiwi kutoza faini baada ya kukamata gari.

Trafiki aeleze sababu

“Akisimamisha gari ni lazima akueleza sababu za kukusimamisha; kwamba anataka kukagua nini katika gari lako,” alisema Kamanda Mambosasa baada ya kuombwa na Mwananchi kufafanua kauli yake jana jioni.

“Nilichokimaanisha ni ile kusimamisha gari na kuanza kutafuta makosa bila kueleza sababu ya kukusimamisha.”

Trafiki wamekuwa na tabia ya kusimamisha gari, kuomba leseni na baadaye kuanza kukagua vitu kama stika ya bima, taa, gurudumu, mtungi wa kemikali za kuzimia moto na viakisi mwanga kwa ajili ya kuashiria gari bovu lililosimama barabarani.

Akipata kosa, askari huandika kuanzia Sh30,000 kwa kosa, jambo ambalo limesababisha madereva wengi kuingiwa na hofu kila wanapoona askari hao barabarani.

“Akisimamisha gari ni lazima aeleze sababu za kulisimamisha,” alisema Kamanda Mambosasa kujibu swali “trafiki atatambuaje kama gari lina bima au vitu vingine vya lazima katika gari.

Trafiki atumie busara

Mambosasa pia alisema trafiki pia anatakiwa kutumia busara kumtoza faini mtu ambaye gari lake lina matatizo ya taa kwa kuwa huenda hatumii gari hilo usiku unapoingia.

“Yapo makosa ambayo askari yeyote wa usalama barabarani anayesimamia sheria anaweza kujitathmini mwenyewe na kuona haina ulazima wa kumtoza mtu faini,” alisema.

“Kwa mfano gari langu nimeamua kutembelea mchana tu, ikifika usiku naliegesha. Kuna sababu gani ya kuwa na taa?

“Kwa hiyo ukinikamata kwa kosa la kutokuwa na taa mchana, nitakushangaa kwa kuwa sijavunja sheria. Wakati mwingine askari anapaswa kufikiria uamuzi wa kumtoza faini mchana kwa sababu ya taa.”

Alisema kama ni usiku ni wazi kuwa mhusika atakuwa amefanya kosa.

“Ili tusiingie kwenye malumbano, tunaomba wananchi watii sheria na pale inapotokea udhaifu wa askari kumbambikia kosa mhusika, (mwananchi) anatakiwa kutoa taarifa haraka iwezekanavyo ili hatua zichukuliwe,” alisema.

Aliwataka askari kuacha kutafuta makosa kwa madereva kwa kusimamisha magari na kuanza kuyakagua.

“Unakamata gari halafu unaanza; mara washa taa; mara zima. Tunaendelea kuwaeleza wenzetu kuwa busara inahitajika wakati wa kusimamia sheria,” alisema.

Askari wa pikipiki

Kuhusu polisi kikosi cha pikipiki, Kamanda Mambosasa alisema wana haki ya kukamata gari au chombo chochote barabarani na kukikagua, lakini kuhusu utozaji wa faini jukumu hilo si lao, bali ni la trafiki.

“Anaweza kukukagua lakini linapokuja suala la kutoza faini, hana kitabu. Lazima akupeleke kwa wahusika ambao ni trafiki,” alisema.

Katika maelezo yake Clouds, Mambosasa alisema Jeshi la Polisi ni kwa ajili ya kulinda raia na mali zao, kusimamia sheria na si kukandamiza wananchi.

“Hawana mamlaka ya kutoza faini kwa mtu aliyevunja sheria za barabarani. Jukumu lao ni kumfikisha mtu huyo kwa askari wa usalama barabarani,” alisema.

Alisema kikosi hicho hakikuanzishwa kwa ajili ya kukamata na kutoza faini, bali kupambana na uhalifu. “Kutokana na foleni za Dar es Salaam, polisi ikaona busara kuwaweka askari hao tayari kwa ajili ya kuwahi kwenye matukio ya uhalifu na sio kukamata magari kama wanavyofanya sasa ingawa wanawajibika kushughulikia uvunjaji sheria unapotokea mbele yao,” alisema.

Aliwataka wananchi kutokubali kutoa fedha bila kupatiwa risiti kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kutoa rushwa.

Alisema jeshi hilo linaendelea kuwaelimisha askari wake kusimamia sheria na si kuwaonea watu.

Kauli yake imepokewa vizuri na wadau wa vyombo vya moto.

“Binafsi naona askari wa usalama barabarani wana haki ya kukagua magari kwa kuwa hilo ndilo jukumu lao,” alisema mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kauli ya Mambosasa.

“Lakini nasisitiza kuwe na busara. Lengo si kuumizana, bali ni kuhakikisha sheria zinazingatiwa. Nitoe wito kwa wamiliki kuhakikisha magari yao yapo katika hali nzuri na madereva nao wasiingize magari mabovu barabarani.”

Kamanda Mambosasa pia alifafanua kuhusu tamko la kuzuia nguo fupi, akisema hilo ni kosa la kimaadili na si kisheria na hivyo Jeshi la Polisi haliwezi kulishughulikia kwa kuwa hakuna sheria inayozuia mavazi hayo.   
Share To:

msumbanews

Post A Comment: