Kesi inayomkabili mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM),  Sadifa Juma Khamis imeahirishwa baada ya upande wa Jamhuri kutokamilisha upelelezi.
Leo Januari 18, 2018  mbunge huyo alifika mahakamani ya hakimu mkazi Dodoma akiwa na wakili wake Godfrey Wasonga, kukaa muda mrefu kabla ya kuitwa mahakamani.
Wakili wa Serikali, Biswalo Biswalo ameiambia mahakama kuipangia kesi hiyo siku tarehe nyingine kwa maelezo kuwa upelelezi haujakamilika.
Kwa upande wake, Wasonga amesema hana pingamizi kuhusu kupangiwa tarehe nyingine, kuomba upelelezi ukamilike mapema ili mteja wake aanze kusikilizwa.
Hakimu mkazi wa mahakama ya Dodoma, Mwajuma Lukindo alikubaliana na hoja za pande zote na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 15 mwaka huu.
Desemba 9, 2017, Sadifa alikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akiwa nyumbani kwake Mailimbili mjini hapa akituhumiwa kugawa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa umoja huo.
Mbunge huyo wa Donge na mjumbe wa kamati kuu ya CCM aliyemaliza muda wake, baada ya kukamatwa alilala mahabusu kwa siku tatu baada ya kukosa dhamana.
Mkutano wa uchaguzi wa UVCCM ulifanyika Desemba 10 kuongozwa makamu mwenyekiti wa umoja huo, Mboni Mhita ambaye pia ni mbunge wa Handeni Vijijini.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: