KATIBU wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), Alophance Myunga amenusurika kifo baada ya kitu chenye mlipuko kurushwa dirishani kwake na kufikia kitandani huku yeye akiwa amelela na kisha kusababisha moto ulioteketeza nyumba anayoishi yote.

Amesema kutokana na kurushwa kwa kitu hicho ambacho kilisababisha mlipuko mkubwa chumbani kwake na kisha moto kuanza kuwaka alichofanikiwa ni kuchukua simu yake ya mkononi tu huku vitu vingine vyote vikiteketea kwa moto.

 Myunga amesema yeye ni moja kati ya wapangaji saba wanaoishi kwenye nyumba ambayo wanaishi na chumba ambacho kilianza kuwaka moto ni cha kwake.

Katibu huyo wa UVCCM Wilaya ya Iringa amesema kuwa kwenye mida ya saa saba usiku akiwa amelala chumbani kwake alisikia dirisha lililopo chumbani kwake likivunjwa.Hata hivyo aliogopa kuchungulia kwani hakujua wanaofanya hivyo wanalengo gani dhidi yake.

Ameongeza wakati anaendelea kutafakari huku akiwa bado yupo kwenye kitanda chake alishangaa kuona amerushiwa kitu ambacho hawezi kukielezea ni cha aina gani lakini ghafla kikaangukia chini na kusababisha kulipuka na moto kuanza kuwaka.

“Naogopa kusema ni kitu aina ya bomu au laa.Maana si mtaalamu wa kutambua aina ya kitu ambacho kimerushwa chumbani.Niseme tu baada ya kitu hicho kurushwa kitandani na kudondokea chini, moto ukaanza kufuka na kisha kulipuka.Nilichofanikiwa ni kuchukua simu na Kompyuta mpakato na kisha kukimbilia nje.

“Nilipotoka nje na wapangaji wenzangu nao wakatoka na kuanza kuulizana nani amefanya tukio hilo.Tayari tumetoa taarifa Polisi jana(juzi) usiku baada ya nyumba kuungua na hivyo tunasubiri watakachobaini kilichosababisha nyumba kuchomwa na waliohusika kufanya tukio hilo,”amesema.

Alipoulizwa anahisi nini baada ya tukio hilo, Myunga alijibu kuwa anachoamini sababu kubwa itakuwa ni mambo ya siasa kwani yeye si mfanyabashara na hana kazi nyingine zaidi ya siasa na siku za karibuni kuna moja ya kiongozi wa kisiasa wa upande wa upinzani alimtishia kwa bastola.

“Mbali ya kunitisha kwa bastola aliniambia kuwa nitakiona na lazima atanihamisha Iringa kwani najifanya mjanja kwa kuwa nimetoka Dar es salaam.Huyu kiongozi(jina tunalo) ndio atakuwa adui yangu namba moja na ndio namhisi atakuwa kafanya tukio hilo.

“Inaonesha kabisa walikuwa wamedhamiria kuniuua mimi na ndio maana walivunja dirisha la chumbani kwangu na kurusha kitu hicho ambacho kilisaabisha mlipuko uliofanya moto kuanza kuwaka.Hata hivyo acha Jeshi la Polisi Iringa nalo lifanye kazi yake ya kuchunguza na ukweli utapatikana,”amesema.

Advertisement
Share To:

msumbanews

Post A Comment: