SERIKALI imetoa masharti ili kuruhusu kuchukuliwa kwa sukari ya viwandani iliyokwama katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuviwezesha viwanda vitano vilivyoagiza visifungwe kwa kukosa malighafi .
Hatua hiyo imefikiwa baada ya juzi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuishauri serikali kuruhusu sukari hiyo iliyokuwa inashikiliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kuchukuliwa ili kuviokoa viwanda hivyo. Viwanda vilivyolalamika sukari yao kuzuiwa na TRA bandarini ni Kiwanda cha Sayona cha Dar es Salaam na Mwanza, Kiwanda cha Ivory cha Iringa, Kiwanda cha Iringa Food Beverage cha Iringa na Kiwanda cha Anjari cha Tanga.
Aidha kiwanda cha Coca-Cola Kwanza Limited cha Dar es Salaam kililalamika kwa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kutotosha kwa sukari waliyoagiza kutokana na kibali kipya walichopewa na hivyo nao kuwa katika tishio la kufunga kiwanda.
Uamuzi wa kupewa masharti ya mikataba kwa viwanda hivyo, ulifikiwa mjini hapa jana katika kikao kilichowajumuisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sadick Murad, Mnadhimu wa Shughuli za Serikali bungeni ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, Jenista Mhagama na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.
Majadiliano hayo pia yalimhusisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyeshiriki kwa njia ya simu na baadaye kufikiwa uamuzi wa viwanda hivyo kupewa masharti ili kuviwezesha kuchukua sukari yao bandarini.
Akizungumzia masharti yaliyotolewa, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Murad alisema serikali imeamua kuingia mikataba na viwanda hivyo, ambayo itaviwezesha kuchukua sukari hiyo katika kipindi kisichozidi siku tatu kuanzia jana.
Alisema tangu Rais John Magufuli alipotoa agizo kwa viwanda vinavyotumia sukari kama malighafi ya uzalishaji kwa bidhaa zao mwishoni mwa mwaka jana kama njia ya kuwadhibiti wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoagiza sukari hiyo na baadaye kuiuza kwa wananchi, ni viwanda tisa tu vilivyohakikiwa na kupewa vibali vipya. Kuhusu Coca-Cola alisema kiwanda hicho kilifanyiwa uhakiki na kupewa kibali cha kuagiza sukari kulingana na mahitaji waliyoyaainisha lakini sasa wanalalamika kuwa sukari waliyoagiza imekwisha na wanaomba waruhusiwe kuagiza nyingine, hatua ambayo inalazimisha kiwanda hicho kufanyiwa uhakiki upya ili kujua mahitaji yao halisi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: