FAMILIA ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu imewaomba Watanzania kuendelea kumchangia fedha za matibabu kwani haijapata msaada wa serikali wala Bunge huku gharama za kumhudumia zikiwa kubwa.

Akizungumza mwanzoni mwa wiki na mwandishi wetu kwa njia ya simu, mdogo wa Lissu, Vicent Mghwahi, alisema tangu Serikali itoe ahadi ya kumtibu Lissu (Chadema) kokote ndani au nje ya nchi, kasi ya uchangiaji imepungua huku gharama za matibabu zikiendelea kuongezeka.
Lissu alihamishwa kutoka Hospitali ya Nairobi Januari 6 kwenda Ubelgiji kwa matibabu zaidi, baada ya kulazwa nchini Kenya kwa miezi minne.

Mghwahi alisema kwa wastani matibabu ya ndugu yao yanagharimu hadi Sh. milioni 100 kwa mwezi akiwa nchini humo na kutokana na gharama hizo kuzidi kupaa, wanajipanga kufanya harambee ili kukusanya fedha.

"Tunachofanya kwa sasa tunawasiliana na marafiki mbalimbali, ndugu na jamaa ambao wanaendelea kutoa michango yao ambayo inatusaidia Lissu kupata matibabu," alisema.
Alisema hadi sasa Bunge halijatoa fedha ambazo ni stahili za Lissu kwa ajili ya matibabu, na kwamba kumekuwa na majibizano ya barua ambayo hayajazaa matunda.

Bunge limekuwa likidai kuwa Lissu hakufuata utaratibu rasmi kufuata matibabu nje ya nchi baada ya kutolewa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Septemba 7, mwaka jana.
Lissu (49) anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Ubelgiji baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: