Kuchunwa ni ile hali ya mwanaume kugeuzwa ‘grisi’ au kitega uchumi na mwanamke ambaye si mke wako lakini mna mahusiano yanayofanana na hivyo kwa namna moja ama nyingine.
Kwa miaka kadhaa sasa wanaume tumeishi tukichunwa, huku kila mmoja wetu anayepata fursa ya kuzungumzia suala hili, amekuwa akigusia kuhusu hasara zake tu.
Lakini falsafa zinasema, kila chenye hasara kina faida pia, hivyo hata kuchunwa kumegubikwa na faida lukuki ambazo huenda tumeamua kutozitazama tu.
Faida ya kwanza ya kuchunwa ambayo hatupaswi kuibeza, ni vile ambavyo kuchunwa kunamfanya mwanaume awe mbunifu katika kutafuta pesa. Kwa mfano, ulishawahi kukumbana na mwanamke aliyejaaliwa kipaji cha kuchuna, akakukwangua kila kitu na kukuacha sifuri kiasi kwamba ukawa unaona fursa ya kupata pesa katika kila unachokiona na kukisikia.
Kwa mfano, hili zoezi la kukamatwa wavaa nguo fupi na wanyoa viduku, Watanzania wote tunaweza kuwa tunalichukulia kama operesheni ya kunyoosha maadili tu, lakini wewe peke yako ukawa na maono ya mbele zaidi na ukaona fursa ya kupata hela humohumo ndani; unawaza kwamba itakuwaje ukipata tenda ya kuwa unawanyoa vijana wote watakaokamatwa na viduku? Au wadada wanaokamatwa na vimini, wanyang’anywe, halafu wewe uvinunue kwa bei ya kutupa, na ukaviuze Nairobi Kenya ambako bado vina soko? Huwezi kuwa na mawazo ya hivi bila kuchunwa kisawasawa.
Pia, kuchunwa kunasaidia sana kunusuru ndoa. Kivipi? Kafunue vitabu vyote vya dini, soma taratibu, utagundua kuwa kitu kikubwa zaidi kinachotengeneza ndoa imara ni upendo baina ya wanandoa.
Sasa ulishawahi kupita kwenye kumi na nane za mwanamke mwenye shahada ya kuchuna? Akakunyonyoa kila ulichokuwa nacho na kukuacha huna jambo mfukoni? Unapofikia hatua hii, bila hata kulazimishwa unaanza kujikuta unarudisha upendo kwa mkeo hata kama ulikuwa unamkwepa kwepa, kwa sababu yeye ndiye mwanamke pekee hapa duniani ambaye labda anaweza kukupenda na kukurekebishia mambo yako bila kumlipa. Usingechunwa ungemkumbuka lini?
Faida nyingine ya kuchunwa ni vile ambavyo inatufanya tuelewe thamani halisi ya pesa. Unaweza kuwa una manoti mengi kwenye pochi ukajihisi ndiyo una pesa.
Lakini akitokea mwanamke mwenye uzoefu wa miaka mitatu tu wa kuchuna mabuzi, anaweza kumaliza manoti yote uliyokuwa nayo ndani ya saa 24 na kukuacha kwenye hali mbaya isiyoelezeka.
Hapa mwanaume unapata somo kwamba siku nyingine unapokuwa na noti nyingi, unahitaji umakini nazo kwa sababu thamani ya pesa haipimwi kwa wingi wa makaratasi uliyobeba, inapimwa na matumizi yako.
Faida nyingine ya kuchunwa ni vile ambavyo kuchunwa kunarudisha ukaribu kati yetu wanaume na Mungu. Ulishawahi kugundua kuwa unapokuwa na pesa, huwa unakuwa na kakiburi fulani kalikojificha ambako kuna muda kanavuka mipaka kiasi kwamba unamkosoa hata Mungu?
Lakini ukikutana na mtoto wa mjini, akakuchuna unavyostahili na kukukausha kabisa heshima yako kwa Mungu inarudi na anakuwa habanduki moyoni mwako, kila unapokaa mwenyewe unamtaja ndani kwa ndani ukimuomba akupe tena pesa kama zile ulizochunwa huku ukimuahidi kwamba safari hii utazitumia kwa akili sana.
Wanaume tuendelee kufurahia kuchunwa, kuna faida nyingi sana.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: