BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC) limesema asilimia 90 ya malalamiko waliyoyapata, yanatokana na huduma za simu za mkononi ikiwamo wananchi kutuma fedha bila jina kuonekana.
Katibu Mtendaji wa TCRA-CCC, Mary Msuya, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu malalamiko waliyoyapata katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana.
Alisema katika malalamiko hayo, watu wamekuwa wakilalamikia utumaji wa fedha kwenda mitandao mingine bila jina kuonekana kabla ya kutuma jambo, ambalo linawasababishia usumbufu pale wanapokuwa wamekosea kutuma fedha.
Alisema jambo hilo tayari wameliwasilisha Benki Kuu (BoT) ili ichukue hatua kwa wale ambao wanatuma fedha kupitia simu za mikononi kwa majina kuonekana kabia ya kufanyika kwa miamala.
Alisema mbali na suala hilo, pia kumekuwa na matangazo ya michezo ya kubahatisha ambayo hutumwa kwenye simu kinyume cha utaratibu hali ambayo inawakwaza watumiaji wa mawasiliano.
“Utakuta mtu anasubiri ‘message’ (ujumbe) ya maana labda anategemea kupokea muamala wa fedha. Matokeo yake inakuja ‘message’ ya ‘cheza biko’ au ‘tatu mzuka’. Kama mtu kacheza mara moja basi haina haja ya kuendelea kumtumia ‘message’ kila mara au waweke ‘option’ (nafasi) ya mtu kujitoa au waweke matangazo yao katika magazeti na si kuwasumbua watumiaji wa simu za mikononi. Mbali na matangazo hayo ya kubahatisha yapo mengine yanatumwa kinyume cha utaratibu,” alisema.
Aidha, Msuya alisema kwa upande wa huduma za utangazaji, malalamiko yalihusu kutokupatikana kwa chaneli za bure za kitaifa kupitia huduma ya digitali mpaka mtumiaji alipie kinyume cha kanuni zinazotaka apate huduma hizo bure bila gharama yoyote.
Alisema licha ya serikali na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuchukua hatua, bado watumiaji wanapata changamoto ya kutakiwa kuongeza fedha ili kupata king’amuzi kingine ili kuona chaneli za bure tofauti na ilivyokuwa awali.
“Baraza linapenda kutoa rai kwa watoa huduma kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa za kutosha kwa watumiaji ili kuwawezesha watumiaji kufanya maamuzi sahihi na kupata huduma inayostahili.
"Watumiaji wa ving’amuzi vya StarTimes wangepewa taarifa ya kutosha wakati wa kununua ving’amuzi malalamiko yaliyopo sasa yasingekuwepo,” alisema Msuya.
Aidha, Msuya alisema kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano zinatakiwa kutoa ushirikiano kwa baraza katika kushughulikia malalamiko ya watumiaji kwa muda muafaka.
Post A Comment: