Mkuu wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Martha Mkupas ametishia kuyafunga machimbo ya Nyakafulu wilayani humo iwapo vurugu za kuhatarisha amani zitaendelea ambapo alisema amelazimika kutumia jeshi la polisi kuwatuliza wachimbaji waliokuwa wakipinga unyanyasaji unaofanywa na kikundi cha Isanjabadugu kinachosimamia shughuli za uchimbaji kwenye eneo hilo.

Mkupas amesema atayafunga machimbo hayo iwapo vurugu hizo zitaendelea ambapo wachimbaji hao wanazifanya kwa madai kikundi cha Isanjabadugu kinatumia vyombo vya dola ikiwemo polisi kuwapora mawe yenye madini kwa kusingizia gharama za uchimbaji ambapo katika mifuko 100 ya mawe kikundi hicho huchukua mifuko 30.

Hata hivyo mmoja wa wachimbaji hao Sabuni Jasaga amesema wachimbaji wanadhurumiwa mali zao na kikundi hicho ambacho hakitumii gharama zozote na badala yake wachimbaji wanapofanikiwa kupata mawe huchukua kwa nguvu asilimia 30 huku wamiliki wa mashamba wakiambulia asilimia 5 hali ambayo inapingwa na wachimbaji hao.

Kufuatia hali hiyo afisa madini mkazi kanda ya Geita Ally Said amesema mgogoro huo wa kupinga kikundi hicho kuendelea kuwapokonya mawe hayo ya madini tayari mkoa unatafuta namna ya kumaliza bila kuleta madhara ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani kwenye eneo hilo.

Jana wachimbaji hao waliandamana wakipinga kikundi cha Isanjabadugu kuendelea kukusanya mawe hayo hali ambayo mkuu wa wilaya ya Mbogwe Mkupas aliamuru polisi kuwatawanya wachimbaji hao kwa mabomu ya machozi wakati wakijaribu kuishambulia kambi ya kikundi hicho.

Mmoja wa viongozi wa kikundi hicho Evarist Gervas amekiri kukusanya mawe hayo kwa madai ni makubaliano waliowekeana na wachimbaji ingawa afisa madini kanda ya Geita Said amesema eneo hilo wote waliopo sio la kwao bali ni eneo la kampuni ya Mabangu Miners Ltd ambao kabla ya wachimbaji hao walikuwa wakifanya utafiti.
Na Shija Felician - Mbogwe

Share To:

msumbanews

Post A Comment: