raw1
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akiongea na wakazi wa Kanyonza Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50.
raw2
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia) akimsikiliza Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza (kulia), inayojenga barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma.
raw3
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiangalia nodo zinazoshikilia moja ya madaraja yanayojengwa katika barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma.
raw4
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoka kukaguzi wa moja ya madaraja yanayojengwa kwenye barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma.
raw5
Muonekano wa kalvati katika barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma.
raw6

Muonekano wa barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma. Barabara hiyo kwa sasa imefikia asilimia 18 ya ujenzi wake.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameipa miezi minne Kampuni ya ujenzi ya Nyanza Road Works kuongeza kasi ya  ujenzi wa barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 kukamilika kwa wakati na wananchi wa Kibondo na maeneo ya jirani kuweza kuitumia.

Waziri Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo wilayani Kakonko mkoani Kigoma mara baada ya kukagua barabara hiyo na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake.

“Mwezi wa pili mwakani nitarudi hapa kukagua tena maendeleo ya ujenzi wa barabara hii sababu bado kasi mnayokwenda nayo hainiridhishi na kampuni hii ni ya kizalendo ambayo ilitakiwa kuwa ya mfano”, amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amemsisitiza mkandarasi huyo kuzingatia viwango bora vya ujenzi wa barabara kama ilivyosainiwa kwenye mkataba na kumtaka kuzingatia thamani ya fedha katika ujenzi anaoufanya.

“Rafiki yangu ni yule anayefanya kazi vizuri hata kama awe mwanangu kama hafanyi kazi vizuri nitamfukuza”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Naye, Mkandarasi wa kampuni hiyo Bw. Atul Ramji ameahidi kutii na kulifanyia kazi agizo la waziri huyo na kusema kuwa ifikapo mwezi wa pili mwakani ujenzi utakuwa umepiga hatua kubwa.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma amesema ujenzi wa barabara hiyo kwa sasa umefika asilimia 18  kutoka asilimia tano zilizokuwepo awali ambapo kwa sasa kazi zinazofanyika ni ujenzi wa makalvati katika barabara hiyo.

Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amemuagiza mkandarasi wa kampuni hiyo kuanza mara moja kuipatia huduma ya maji Shule ya Sekondari ya Kanyonza angalau mara moja kwa wiki kutoka kwenye kambi ya ujenzi wa barabara wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu.

Prof. Mbarawa amechukua hatua hiyo baada ya wananchi wa kijiji cha Kanyonza  kumsimamisha na kumueleza changamoto ya Shule ya Sekondari hiyo iliyopo katika kijiji hicho wilayani Kakonko kukabiliwa na uhaba wa maji hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilometa nne kufuata huduma hiyo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: