Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye ameahidi
kutoa shilingi laki tano kwa kila goli litakalofungwa na timu ya
Serengeti Boys katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la
mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 utakaofanyika
kesho katika Uwanja wa Taifa dhidi ya Congo-Brazzaville.
Akiongea
na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Nape amesema milango
ipo wazi kwa wadau wengine wa michezo kujitolea katika kuiwezesha timu
na hivyo kufanya vizuri katika mechi hii ambayo ni muhimu sana kushinda
ili kufuzu kwa fainali hizo.
“Hii timu ni yetu sote hivyo
inahitajika tuimiliki, tuepe nguvu, tuiombee ili iweze kufanya vizuri na
hatimaye kufuzu kuingia fainali kwa kuitoa timu ya Congo-Brazzaville”
amesema Nape.
Ameongeza kuwa kesho asubuhi atakutana na
wachezaji wa timu hiyo ili kuwapa maneno ya faraja kabla ya kuanza kwa
mechi na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa
motisha wachezaji kwa kuwashangilia na kuwatia moyo.
Mbali na
hayo Waziri Nape ametoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya kadi za
kieletroniki zilizozinduliwa hivi karibuni kwa kueleza kuwa kadi hizo
bado hazijaanza kutumika rasmi ili zitaanza kutumiwa katika mchezo baina
ya Wabunge wa Simba na Yanga pamoja na Bongo Fleva.
Timu ya Serengeti Boys inaundwa na vijana wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 17 ambapo katika mchezo wa kesho watahitaji ushindi na baadaye kufanya mechi ya marudiano mnamo Oktoba 2 mwaka huu nchini Congo-Brazzaville.
www.msumbanews.blogspot.com
Post A Comment: