Waziri wa Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akizungumza na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wakati akifungua kikao kazi cha 17 cha Maafisa hao kinachofanyika Jijini Tanga leo tarehe 9 Mei 2022

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akizungumza na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wakati wa ufunguzi wa  kikao kazi cha 17 cha Maafisa hao kinachofanyika Jijini Tanga leo tarehe 9 Mei 2022
Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa katika kikao kazi cha 17 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kinachofanyika Jijini Tanga leo tarehe 9 Mei 2022

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza katika kikao kazi cha 17 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kinachofanyika Jijini Tanga leo tarehe 9 Mei 2022




Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Waziri wa Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (hayupo pichani) wakati wa Ufunguzi wa kikao kazi cha 17 cha Maafisa hao kinachofanyika Jijini Tanga leo tarehe 9 Mei 2022


Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kuhuisha  taarifa za Serikali kwenye tovuti za Serikali na mitando ya kijamii ili wananchi waweze kupata taarifa na kujua kinachoendelea kuhusu Serikali yao.

Akizungumza leo jijini Tanga wakati akifungua Kikao cha 17 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali, Waziri Nape amesema kuwa Maafisa Habari wa Serikali ni daraja linalorahisisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, hivyo ni muhimu kutimiza  wajibu wao kwa kuwa na taarifa sahihi za Serikali na kwa wakati katika tovuti za Wizara au Taasisi zao.

“Natoa siku 14 kuanzia Mei 14 mwezi huu kila tovuti ya Serikali  na mitandao ya kijamii iwe  na taarifa za Serikali zinazoendana na wakati kuhusu utekelezaji wa Sera au miradi mbalimbali ya Serikali, Afisa atakayeshindwa kutekeleza hili tutaachana nae”, amesema Mheshimiwa Nape

Aidha, akiwa katika kikao hicho Waziri Nape ameiagiza Idara ya Habari – MAELEZO kuandaa mfumo utakaowezesha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano nchini kupatiwa mafunzo kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini ili waweze kuwa na uelewa na kuweza kuisemea miradi hiyo, kuandaa mfumo wa Maafisa Habari kujadiliana masuala mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya kisasa pamoja na kuwa na mfumo wa kupima utendaji kazi wa Maafisa hao.

Katika hatua nyingine, Waziri Nape ameahidi kutatua changamoto ya uhaba wa Maafisa Habari katika ngazi ya Wizara na Halmashauri ili kuhakikisha Serikali ina wataalamu wa kuisemea katika ngazi hizo.

“Nawaahidi hili liko ndani ya uwezo wangu la kusaidia kupata Maafisa habari katika mikoa ya Lindi, Manyara, Mbeya na Tabora na mikoa ya Dodoma, Kigoma na Geita mbayo Maafisa Habari wake wamekuwa Wasaidizi wa Wakuu wa Mikoa. Dodoma.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Kikao Kazi hicho kitandaa mkakati na kujifunza namna ambavyo dunia itahabarika kupitia Tanzania na kufikisha ujumbe wa maendeleo na namna ya  watu kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Pia Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa kuwa lengo la kikao  kazi hico cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini ni  kujengeana uwezo wa namna bora ya kuisemea Serikali na kuwa atahakikisha maagizo yote yaliyotolewa yanatekelezwa ili kutimiza jukumu hilo kwa ufanisi.
Share To:

Post A Comment: