Serikali imewataka wananchi kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi yanayoweza kusababisha maafa kama vifo, uharibifu wa miundo mbinu na mazingira nchini.

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya wakati wa kikao cha Baraza la Usimamizi wa Maafa kilichokutanisha Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo ni wadau wa usimamizi wa maafa na wataalam katika ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa ipo haja ya wananchi kupewa elimu kupitia wataalamu mbalimbali kuhusu dhana ya usiammaizi wa maafa na namna ya kuzuia madhara ya maafa au kuchukua hatua ya kujiokoa pindi yanapotokea.

“Tunahimiza tufuate maelekezo ya wataalamu kwa kutojenga kwenye maeneo ambayo hayafai hasa ya mabondeni, kujiepusha na kulima maeneo ya vyanzo vya maji na wafugaji kutokuwa na mifugo mingi ambayo anashindwa kuihudumia hatimaye tatizo likitokea la ukame anashindwa kuwapa huduma bora,”alisema Bw. Mmuya.

Pia akizungumzia kuhusu hali ya hewa aliwahimiza wakulima nchini kuzingatia utabiri wa hali ya hewa ambao umekuwa ukitolewa na wataalam ili kujua mazao rafiki ya kulima kwa msimu husika.

“Tuangalie mabadiliko ya hali ya hewa tuweze kulima kulingana na hali ya hewa na elimu hii itatolewa kwa wakulima kama kipindi cha mvua nyingi tunatakiwa kulima nini na wakati wa mvua chache tulime nini elimu hii itatolewa maeneo yote,”alieleza.

Aidha kuhusu sera alibainisha kwamba ofisi hiyo kama wasimamizi wa sera na wasimamizi wa maduhuli katika kila wizara hazina budi kuweka bajeti itakayosaidia  kukabili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Kwa sisi  wasimamizi wa sera na waduhuli katika kila wizara kujaribu kuweka bajeti kila wizara ili tatizo linapojitokeza tuwe na mpango wa muda mfupi kutekeleza changamoto zinatokana na mabadiliko ya hali ya hewa,” alibainisha Bw. Mmuya.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga alisisitiza sekta mbalimbali zinazohusika na uhifadhi wa chakula na uokoaji kuweka mikakati thabiti itakayosaidia kudhibiti maafa na kuyakabili pindi yanapojitokeza.

Share To:

Post A Comment: