TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Arusha imewapandisha kizimbani vigogo sita wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA), wanaokabiliwa na mashtaka  ya  matumizi  mabaya ya madaraka, kula njama na kujipatia manufaa ya fedha kiasi cha Shilingi bilioni 5.3 kinyume cha sheria.

Kati ya vigogo hao waliopandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, kujibu mashtaka yanayowakabili ni aliyekuwa Mkurugenzi wa AUWSA, Mhandisi Ruth Koya.

Katika shauri hilo, washtakiwa ambao wapo saba mbali na Mhandisi Ruth Koya, pia yupo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Kiure Engineering LTD, Omari Kiure, ambaye ni mkazi wa jijini Arusha.

Washtakiwa wengine waliopanda kizimbani ni Benedict Kitigwa,James Mwambona,Steven Msenga , Godfrey Macha na Juma Mkwawa ambao wote wakiwa ni watumishi wa mamlaka hiyo ya maji AUWSA  jijini Arusha.

Akisoma mashtaka hayo, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Herieth Mtenga, Mwendesha mashtaka wa (TAKUKURU) Violet Machali, alidai washtakiwa hao, kwa pamoja walitenda makosa manne ya uhujumu uchumi na kujipatia fedha kiasi cha Shilingi bilioni 5.310,823,214 kinyume na sheria.

Alidai mahakamani hapa, kuwa kosa la shtaka la kwanza linawahusu washtakiwa wote kwa pamoja kwa kuwa kati ya Desemba, 2017 na Oktoba mwaka 2018, katika eneo la Jiji la Arusha, washtakiwa hao walikula njama kupitia mradi wa maji wa Kanda na kujipatia manufaa isiyostahili kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Kiure Engineering LTD  bila kufuata taratibu za manunuzi.

Mwendesha mashtaka huyo, alidai kwamba shtaka la pili ni  matumizi mabaya ya madaraka na shtaka hilo linamkabili mshtakiwa wa kwanza  Mhandisi Ruth Koya, ambaye anadaiwa akiwa mtumishi wa umma na akijua kwamba ni kosa kisheria,aliiwezesha kampuni ya Kiure Engineering LTD, kupata mkataba wa ujenzi wa ofisi za Kanda za Mamlaka hiyo, kitendo hicho kilisababisha kampuni hiyo kupata manufaa ya fedha kiasi cha Sh.bilioni 5.3 kinyume cha sheria ya manunuzi ya mwaka 2011kifungu cha 36(5).

Violet, aliieleza mahakama hiyo, kiwamba shtaka la tatu na la nne linamkabili mshtakiwa wa kwanza,1,2,3,4 na 5 ambao ni (Ruth Koya), mshtakiwa wa pili(Benedict Kitigwa) , mshtakiwa wa tatu(James Mwambona),mshtakiwa wan ne(Steven Msenga)  na mshtakiwa wa tano(Godfrey Macha).

Ilidaiwa mahakamani hapa, kuwa kati ya mwezi Desemba 2017 na Oktoba 2018 wote kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao na kupelekwa kwa Kampuni ya Kiure Engineering LTD   kupata manufaa ya fedha kiasi cha Sh.bilioni 5.3.

Baada ya mwendesha mashtaka kusoma mashtaka hayo ,aliieleza mahakama hiyo kwamba upande wa Jamhuri hautakuwa na pingamizi la dhamana iwapo mahakama itaona kama inafaa washtakiwa hao kupatiwa dhamana.

“Mheshimiwa Hakimu sisi upande wa Jamhuri hatuna pingamizi la dhamana tunaomba tarehe nyingine, Kwa ajili ya washtakiwa kuwasomea maelezo ya awali kwa kuwa upelelezi wa shauri hili umekamilika,”Alisema Violet.

Kwa upande wake Hakimu Mtega, alisema dhamana kwa washtakiwa hao, ipo wazi na kwamba watapaswa kuwa wadhamini wawili akiwamo mtumishi wa umma mwenye kitambulisho na barua ya utambuzi kutoka kwa mwajiri wake, na Mdhamini atasaidi bondi ya mali  isiyohamishika yenye thamani ya shilingi milioni 20.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanatetewa na Wakili Robert Rogati, na wote walitimiza masharti hayo, na wapo nje Kwa dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa tena kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali Septemba 9 mwaka huu.

Hakimu wa mahakama hiyo, aliahairisha kesi hiyo hadi Septemba 9 mwaka huu,  itakapotajwa tena kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Share To:

Post A Comment: