Na Joachim Nyambo,Mbeya.


 


KUWEPO kwa idadi kubwa ya watoto wakiwemo wa madarasa ya awali wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imeonekana kuwafurahisha wanahabari wanawake waliotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni kwa lengo la kushiriki jjitihada za Serikali za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.


 


Kwa mujibu wa Afisa Uhifadhi wa Hifadhi ya Ruaha, Kitengo cha Utalii, Ahmed Nasoro tofauti na awali kwa sasa mwitikio wa watoto kutembelea hifadhi hiyo ni mkubwa na kwamba wengi wa wanaofika hapo ni wanafunzi wa shule za Awali, Msingi na Sekondari.


 


Nasoro aliwaambia wanahabari hao 31 wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini kuwa zaidi ya watoto 20 wakiwemo walio na umri wa kati ya miaka mitano hadi 15 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakitembelea hifadhi ya Ruaha kila mwezi kwa lengo la kujionea na kujifunza kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo wanyama na mimea.


 


Kutokana na hatua hiyo wanahabari hao wakizungumza na Mtandao huu katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani,Septemba 27 waliipongeza Serikali kupitia taasisi zake na wadau ambao wamekuwa wakijishughulisha na kuvitangaza vivutio vya utalii nchini na pia kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutembelea vivutio.


 


Walisema hatua ya watoto wadogo kuanza kutembelea Hifadhi za Taifa ina manufaa makubwa katika maisha yake na Taifa lake kwakuwa kadiri anavyoendelea kukua atakuwa balozi mzuri wa kuvitangaza vivutio alivyovitembelea na kuwa mfano wa kuigwa na watu wengine.


 


Mmoja wa wanahabari hao,Mary Mwakibete alisema hatua ya mtoto alieye darasa la awali au la kwanza kujifunza kwa vitendo kunamjenga kupenda zaidi masomo na pia kumwongezea ari ya kujifunza.


 


“Binafsi nilijisikia vizuri sana kuona siku hizi mtoto haishii kujifunza kwenye kitabu pekee masuala ya vivutio na rasilimali tulizonazo nchini.Ukisema Tembo anamuona kwa uhalisia.Si kama enzi zetu wanyama kama Pundamilia tuliishi kuwaona kwenye vitabu.Kimsingi inawajenga watoto kuja kuwa watalii wazuri watakapokuwa.” Alisema Mary.


 


Mwanahabari mwingine Ester Macha kwakuwa watoto ni wasimuliaji wazuri wa kile walichokiona na muhimu juhudi za kuendelea kuhamasisha taasisi zinazowalea au kuwafundisha kuweka mikakati kabambe ya kuwapeleka kwenye vivutio ili wanaporudi wawaeleze wenzao waliobaki nini walikiona na kuwapa hamasa.


 


Mwanahabari Matha Sambo alisema alifurahishwa zaidi kusikia miongoni mwa watalii wanaofika hifadhini hapo ni watoto na idadi yao inazidi kuongezeka siku hadi siku na akasema ni funzo kwa wazazi wengine.


 


“Zamani tulizoea na kudhani kuwa wanaopaswa kutembelea vivutio vilivyopo ndani ya nchi yetu ni wazungu au wageni pekee kutoka nje ya nchi.Na kama siyo wazungu basi ni watu wazima,lakini kumbe  hata watoto wanayo nafasi ya kutembelea vivutio vilivyopo katika nchi yao na wakajifunza mambo mbalimbali.” Alisisiza Martha.


 


Grace Mwakalinga yeye alishauri wazo lililoelezwa na  Afisa Uhifadhi Kitengo cha ujirani mwema, Hifadhi ya Taifa Ruaha, Emaculata Mbawi juu ya kuandaliwa Tuzo na kutolewa kwa wananchi ili kuhamasisha utalii akitaka nguvu kubwa ya mpango huo ielekezwe kwa watoto ili kuwapa hamasa zaidi.


 


Hivi karibuni akizindua wiki ya Utalii katika hafla fupi iliyofanyika Septemba 22 ikiwa ni mwelekeo wa siku ya kilele cha siku ya Utalii Duniani Septemba 27,Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Juma Homera alisisitiza jamii kuwafundisha watoto tangu wangali wadogo umuhimu wa kuthamini vitu vya kwao.


 


Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya Utalii duniani mwaka huu ni Utalii kwa maendeleo Jumuishi.


 



Share To:

Post A Comment: