Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo,akizungumza kwenye kikao cha Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake kilichofanyika  April 10,2021 jijini Dodoma,kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Exaud Kigahe (kulia) ni Katibu Mkuu wake Bw. Dotto James.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo,akifafanua jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake kilichofanyika April 10,2021 jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe ,akieleza jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kilichofanyika April 10,2021 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Dotto James akizungumza wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kilichoongozwa na Waziri Prof,Kitila Mkumbo kilichofanyika April 10,2021 jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdallah,akizungumza wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kilichofanyika April 10,2021 jijini Dodoma.

Sehemu ya watumishi wakifatilia hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (hayupo pichani) wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kilichofanyika April 10,2021 jijini Dodoma.


Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo ,amewataka watumishi wa Wizara yake wote nchini kuimarisha sekta ya viwanda na biashara ili kukuza uchumi nchini na kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26.

Prof.Mkumbo ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo,amesema kuwa majukumu ya wizara hiyo ni kutoa mwelekeo na utekelezaji wa kuinua uchumi wetu.

Prof.Mkumbo amesema kuwa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 ni kuona Tanzania inahitimu na kuondoka kuwa nchi masikini inayotegemea kilimo na uchumi wa uzalishaji duni na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 hivyo Wizara ina mchango mkubwa katika kufanikisha azma hiyo.

“Uchambuzi wa maudhui ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26 unaonesha wazi kabisa nafasi ya Sekta ya Viwanda na Biashara,sisi kama Wizara tunatarajiwa kutoa mchango karibu kwa kila eneo la matokeo tarajiwa.”

Aidha amesema pia katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26, malengo sita kati ya mahsusi 12 yanahusu sekta ya viwanda na biashara, kati ya vipaumbele vitano vya mpango huo vitatu vinahusu wizara hiyo, katika Sekta 30 za mpango huo Sekta 6 zinahusu Wizara na katika hatua 156 hatua 54 zinahusu Wizara ya Viwanda na Biashara.

“Taasisi zote zilizochini ya Wizara ya Viwanda zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26, Hivyo nawasihi muendelee kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria Kanuni na taratibu zinazosimamia taasisi zenu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na si kuwa kikwazo”

Hata hivyo, Prof.Mkumbo amesema kuwa hakusudii kutumia muda mwingi katika kutunga Sera, Sheria na mikakati na kuwa yeye analenga katika utekelezaji na kuona matokeo ya utekelezaji huo kwa kuchochea ukuaji wa haraka wa Sekta ya Viwanda na Biashara.

Prof.Mkumbo amewataka wataalamu wa Idara ya Sera na Mipango ya Wizara kusimamia uhuishaji wa nyaraka mbalimbali za kisera na sheria ili ziende na wakati na kuakisi maudhui ya Mpango wa tatu wa Maendeleo na maono ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Prof.Mkumbo amesema kuwa tunataka kuviendeleza viwanda hapa nchini lazima kuwa na kanzi data ya kisasa ya viwanda kwa kuzingatia kiwango cha uzalishaji na ajira, kuweka mazingira na masharti rahisi katika kukuza na kuchochea viwanda vidogo vidogo vinavyotumia teknolojia rahisi na ya kisasa na vilivyojikita vijijini na mijini,

Aidha Waziri Mkumbo ameongeza kuwa lazima tuwawezeshe na kuwahudumia wawekezaji katika viwanda vikubwa na vyenye tija katika uchumi na kuhuisha Mkakati wa Viwanda nchini,ikiwemo dhana ya EPZ na SEZ.

Amesema pia kusimamia kwa karibu miradi ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Taifa ambayo ni mradi wa Chuma wa Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda wa Engaruka, ujenzi wa Kiwanda cha Sukari-Mkulazi na kanda Maalum za Uchumi na Maeneo Maalum ya Uwekezaji

Prof.Mkumbo amesema kuwa kuimarisha utafiti na matumizi yake katika maendeleo ya viwanda, ikiwemo kuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi za utafiti na elimu ya juu na kupanua na kuboresha mahusiano na ushirikiano na taasisi za sekta binafsi.

“Naomba tumeimarisha ushirikiano na OR-TAMISEMI katika maendeleo ya viwanda vidogo vidogo, tunataka kuona uwezekano wa kuwaongeza majukumu maafisa biashara wa Halmashauri ili pia wasimamie viwanda vidogo vidogo katika maeneo yao kwa kushirikiana na SIDO.”amesema Prof.Mkumbo

“Tunataka tunapokutana na wafanyabiashara tufanye mazungumzo yenye tija ya kubadilisha mikakati ya kukuza biashara na masoko, badala mikutano hiyo kutumika tu kama jukwaa la kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara.”

Pia naomba tuendelee kuzipitia kanuni za mamlaka za udhibiti zinazoonekana kukwamisha biashara, kuchochea na kuhamasisha tabia ya kujali wateja miongoni mwa watendaji wa Serikali wanaohudumia sekta mbalimbali za biashara.

Aidha, Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa kuna haja ya watendaji wa wizara na taasisi kubadilisha mtizamo katika utendaji kazi na kuwa na “corporate thinking” na tabia ya kujali wateja kwa kuzingatia kuwa wadau tunaowahudumia ni wafanyabiashara.

Waziri Mkumbo amewataka wataalamu wa wizara hiyo kuhakikisha wanatoa ushauri wa kitaalamu wenye ushahidi wa kisayansi na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa wafanyabiashara

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: