Nteghenjwa Hosseah - Dodoma


Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI     

Dr.Festo Dugange amekabidhi kadi za bima ya Afya ya jamii iliyoboreshwa (iCHF) kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa niaba ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Nchini kote mapema leo Jijini Dodoma.


Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi waliopatiwa Kadi za CHF wanatoka katika kaya zipatazo 361,539 kutoka katika Mikoa 24 Tanzania bara.


Akizungumza katika Hafla hiyo Mhe Dugange amewashukuru wadau waliowezesha upatikanaji wa Bima hizo za Afya ya Jamii kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwataka zoezi hilo kuwa endelevu ili watoto hao waweze kuwa salama wakati wote.

 

“Napenda kuwashukuru wadau wetu, Shirika la Maendeleo la Marekeni (USAID) kwa msaada mkubwa wanaotoa kwa Serikali kuwahudumia watoto walio katika mazingira hatarishi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo huu wa USAID Kizazi kipya unaotekelezwa na Shirika la Pact ambao ndio uliofanikisha upatikanaji wa Bima hizi za Afya ya Jamii” alisema Dr. Dugange.


Mradi huu wa USAID kizazi kipya katika kipindi chake cha miaka minne umekuwa na manufaa makubwa, watoto wetu walio katika mazingira hatarishi zaidi ya laki saba wamenufaika kwa kupata vifaa vya shule, mafunzo ya ufundi, vifaa vya kuanzia biashara na huduma za afya na VVU/UKIMWI alisema.


Upatikanaji wa Bima za Afya kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kaya zao ni msaada wenye tija sana kwetu kwa kuwa sasa familia hizo zina uhakika wa kupata huduma za Afya katika kipindi chote cha mwaka bila kuwa na wasiwasi wowote alisisitiza Dr Dugange.


Pia Dr Dugange aliwataka wataalamu wa Afya nchini kote kuhakikisha kuwa familia zilizopatiwa Kadi za Bima ya Afya ya Jamii na wanachi wote kwa ujumla walio katika mfumo wa Bima hii wanapata huduma za Afya bila shida yoyote.


“Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote Nchini mnaelekezwa kusimamia mfuko huu na kuhamasisha wananchi wote kujiunga na CHF iliyoboreshwa.


“Sasa CHF iliyoboreshwa iwe agenda ya kudumu katika vikao vyote vya kiutawala katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuleta mwamko kwa wananchi wote kujiunga na mfuko huu waweze kunufaika na kitita cha mafao kinachopatikana kupitia CHF” alisisitiza Dr Dugange


Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Dr.Ntuli Kapologwe amesema msaada huo umegharimu shilingi Bil 4.6 fedha kutoka shirika la Pact-Tanzania.


“Fedha hizo mbali na kunufaisha watoto waliokatika mazingira hatarishi na kaya zao kwa kupata huduma za Afya mwaka

Mzima pia zitawezesha vituo kuboresha huduma za Afya ikiwemo kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba” alisema Dr Ntuli.


Aliongeza kuwa wanachama wanaoenda kupata kadi za CHF kupitia msaada huu wanaongeza idadi ya wanachama kutoka asilimia 5.5 iliyopo hivi sasa hadi kufikia asilimia 10.


Mwisho

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: