Na Mwandishi Wetu Kondoa

Katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Serikali imesema itaendelea kupambana na unyanyasaji wa Wazee nchini ikiwemo kudhibiti vitendo vya mauaji ya Wazee.

Hayo yamesemwa Wilayani Kondoa mkoani Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Afya-. Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa  Siku ya Wazee kwa Mkoa huo.

Aidha Dkt. Jingu ameongeza kuwa Serikali inafanya jitihada za kuwatunza Wazee hasa wasiojiweza kwa kuboresha makazi ya Wazee yanayosimamiwa na Serikali.

"Jamii tumewasikia Wazee wetu ni jukumu letu kuwalinda wazee hawa wafurahie maisha na ni wajibu wetu tusiukimbie"

"Hawa wazee nao wakati wanatulea wangesema hawana muda na sisi tungekuwa wapi tungekuwa wakina nani tuwatunze wazee wetu" alisema

Akitoa taarifa ya maboresho ya huduma za Wazee kwa ngazi ya Wizara Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng'ondi amesema Serikali imeendelea kuwatunza wazee wasiojiweza katika Makazi 13 yanayosimamiwa na Wizara kwa kuwapatia huduma stahiki kwao.

"Tunahudumia wazee 281 mpaka sasa katika Makao haya tunayoyahudumia kwa kuwapatia wazee huduma za Afya na huduma nyingine muhimu" alisema.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Maduka Kesi amesema kuwa Mkoa wa Dodoma umeendelea na jitihada za kuwatunza Wazee kwa kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo huduma za Afya na kuwaasa Jamii kuwajibika kuwatunza.

"Sisi tunaongoza kwa asilimia 25 ya kuwawezesha wazee kujiunga na huduma za Afya kwa kujiunga katika Bima ya Afya iliyoboreshwa ili kuwawezesha kupata huduma Bora" alisema.

Ameongeza kuwa ingawa Serikali inawahudumia wazee  jukumu la kwanza ni kwa jamii kuhakikisha wanawahudumia wazee wao.

Tanzania imeungana na nchi nyingine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wazee ikiongozwa na Kauli Mbiu isemayo: Familia na Jamii Tuwajibike Kuwatunza Wazee.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: