Na John Walter- Manyara

Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dr. Bashiru Ally ameweka Jiwe la Msingi katika  Jengo la Ofisi ya Ccm mkoa wa Manyara lenye thamani ya shilingi Milioni 650.

Jengo hilo la Ghorofa moja ambalo chini lina  ukumbi mkubwa wa mikutano wenye uwezo wa kuingiza watu 1200 hadi 1500, juu vyumba 10 vya ofisi pamoja na ukumbi,  hadi sasa limefikia hatua ya Upauzi  na limegharimu shilingi Milioni 368,907, 286.

Akizungumza baada ya kuweka Jiwe hilo la Msingi Oktoba 25,2020 kwenye jengo hilo ambalo linaendelea kujengwa katika mtaa wa Miomboni kata ya Bagara Mjini Babati, Dr. Bashiru ameupongeza uongozi wa chama Chama Mapinduzi mkoani hapa kwa hatua hiyo muhimu waliyoifikia.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Jacob Siay amesema Ujenzi huo ulianza mwezi Desemba mwaka 2019  ambapo kabla ya kuanza ujenzi, vikao vya chama vilikaa na kuunda kamati ndogo ya ujenzi yenye jumla ya wajumbe 10 ikiongozwa na mkuu wa mkoa aliestaafu Alexander Mnyeti.

Amesema ujenzi huo unatekelezwa kupitia michango mbalimbali ya wadau wa chama cha Mapinduzi kupitia harambee iliyoendeshwa na mkuu wa mkoa Aleaxander Mnyeti kwa kushirikiana na kamati ya ujenzi na uongozi wa chama chini ya Mwenyekiti wa chama mkoa wa Manyara  Simon Lulu.

Amesema Katika harambee Sita zilizofanyika zikihusisha kada mbalimbali za viongozi katika mkoa wa Manyara, walifanikiwa kukusanya jumla ya  Shilingi 443,200,000 ambapo hadi sasa wamekusanya shiling Milioni 311,490,000.

Aidha amesema wanatarajia ujenzi wa jengo hilo kukamilika baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020  wa kuchagua Madiwani, Wabunge na Rais kukamilika.

Mwenyekiti wa chama Cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Simon Lulu amesema Ukumbi huo utaoungezea chama Mapato kwa kuwa utakodishwa kwa shughuli mbalimbali.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara wakishuhudia uwekwaji wa jiwe la Msingi kwenye Jengo la Chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara.


Share To:

Post A Comment: