Na Mary Gwera, Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania,  Prof. Ibrahim Hamis Juma ameutaka Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kuongeza wigo wa mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama kwenye eneo la Teknolojia hususani utoaji haki mtandao ‘e-judiciary, e-justice.’

Akifungua rasmi semina elekezi kwa Wajumbe wapya wa Baraza la saba (7) la Uongozi wa chuo hicho, mapema Oktoba 07 katika Ukumbi wa Shule ya Sheria jijini Dar es Salaam,  Jaji Mkuu amesema kuwa kwa kufanya hivyo, Chuo kitaisaidia Mahakama kutekeleza azma yake ya kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanayoenda kwa kasi na kufanya matumizi ya TEHAMA kuwa ni ya lazima na si hiyari.

“Karne ya 21 imelazimisha mabadiliko mengi na makubwa yanayogusa nafasi ya Mahakama katika utoaji haki, hususani ulazima wa matumizi ya TEHAMA kama nyenzo wezeshi katika utoaji wa haki,” amesema Jaji Mkuu.

 Jaji Prof. Juma ameongeza kuwa Mahakama ina utayari mkubwa juu ya matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma zake, hivyo ni muhimu watumishi wake wakawa na utayari na ujuzi wa matumizi lengo likiwa ni kuwafikishia wananchi huduma ya utoaji haki kwa haraka zaidi.

Aidha, Jaji Mkuu amewaeleza Wajumbe hao kuwa ana imani kuwa Baraza la Uongozi wa chuo hicho litaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania hususani katika eneo la mafunzo ambayo ndio chachu ya mafanikio.

Kwa upande mwingine,  Jaji Mkuu amekipongeza chuo hicho kwa kuendesha mafunzo kwa Maafisa mbalimbali wa Mahakama kuhusu namna bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi. Ametaja Maafisa waliopatiwa mafunzo ambao ni pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Wasajili na Warajisi kutoka Zanzibar, Mahakimu na wengineo.

Pia Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa lengo kuu la kuandaliwa kwa semina hiyo kuwasaidia wajumbe wapya wa Baraza kukifahamu kwa kina chuo.

“Mafunzo haya yameandaliwa ili kutoa nafasi kwa wajumbe wapya kuelewa kwa undani uhusiano uliopo kati ya Mahakama ya Tanzania na Chuo, na matarajio ya Mahakama kwa chuo pamoja na kuliwezesha Baraza kusimamia Menejimenti ya chuo kwa umahiri na ufanisi mkubwa,” ameeleza Jaji Dkt. Kihwelo.

Katika semina hiyo, Washiriki wamewezeshwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo majukumu na wajibu wao, Mabaraza na Bodi za Taasisi za Umma kusimamia Menejimenti, Sheria za fedha za umma yam waka 2001, Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 pamoja na marekebisho ya kanuni zake.

Share To:

Post A Comment: