Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizindua Kamusi ya kwanza ya Lugha ya Alama ya kidijitali ya Tanzania na Mwongozo wa Utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi viziwi wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi  yaliyofanyika Mkoani Tabora.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua Kamusi ya kwanza ya lugha ya alama ya kidijitali yenye lengo la kupunguza changamoto ya mawasiliano katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi viziwi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akionesha kishkwambi chenye kamusi huku Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Magret Komba akionesha Mwongozo wa Utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi viziwi mara baada ya kuzinduliwa katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi yaliyofanyika Mkoani Tabora.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu, Kamisha wa Elimu Dkt. Lyabwene Mutahabwa, Makamu Mwenyekiti CHAVITA wakicheza  na washiriki  ambao ni viziwi  wakati wa  kikele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi yaliyofanyika Mkoani Tabora.
Wanafunzi viziwi wa shule ya sekondari  Kazima iliyopo Tabora wakiimba kwaya mbele ya Mgeni rasmi Dkt. Ave Maria Semakafu (hayupo pichani)wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi yaliyofanyika mkoani Tabora

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua Kamusi ya kwanza ya lugha ya alama ya kidijitali yenye lengo la kupunguza changamoto ya mawasiliano katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi viziwi. 

Akizindua kamusi hiyo Mkoani Tabora, katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi yenye kauli mbiu “Kuhakikisha upatikanaji wa haki za binadamu kwa Viziwi”, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Ave Maria Semakafu amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote yenye ulemavu kupata elimu na huduma nyingine za kijamii. 

Dkt Semakafu amesema pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu, kundi la viziwi lilikuwa limeachwa nyuma huku changamoto kubwa ikiwa ni mawasiliano na kutokuwepo kwa walimu wa kutosha hasa katika ngazi ya sekondari ndio maana imeandaa kamusi hiyo kuwe na lugha moja ya alama na kutoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha katika shule zinazopokea watoto viziwi. 

“Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja ya alama kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo, hivyo itaendelea kusimamia uendelezaji na usanifishaji wa lugha ya alama ili kuwezesha utoaji elimu, kurahisisha ujifunzaji na kuboresha mawasiliano katika jamii.,”alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Nae Kamisha wa Elimu 
Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani ndio mwanzo wa mafanikio katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji nchini kwani ni siku ambayo kamusi ya lugha ya alama ya kwanza nchini tena ya kidijitali inazinduliwa pamoja na mwongozo wa utekelezaji wa mtaala wa elimu ya sekondari kwa wanafunzi viziwi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET)Dkt. Aneth Komba  anasema Taasisi anayoisimamia ndio walipewa jukumu la kuandaa Kamusi hiyo  na kwamba imeandaliwa kwa kufata taratibu zote ikishirikisha wadau wote na kwamba itatumiwa na wanafunzi viziwi kutoka Tanzania Bara na Visiwani. 

Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Magret Matonya amesema uzinduzi wa Kamusi hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini wakiwemo viziwi wanapata elimu bora. Aidha ameongeza kuwa  Wizara imeanza ujenzi wa shule ya mfano ya viziwi  katika Halmashauri ya Masasi Mkoani Mtwara ikiwa ni jitihada za kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji wanafunzi viziwi ambapo ujenzi wake utagharimu bilioni 1.5.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Taifa (CHAVITA) Selina Mlemba amesema wanaishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kwamba wanaamini miaka michache ijayo watapata wataalamu wengi katika maeneo mbalimbali wakiwemo madaktari kwa kuwa sasa wamepata kamusi itakayowawezesha kusoma bila changamoto.

Mtaalamu elekezi wa uandaaji wa Kamusi ya lugha ya alama kutoka Archbishop Mihayo University College (AMUCTA) Profesa Henry Muzale amasema uaandaji wa kamusi hiyo umezingatia changamto zote za viziwi na hii ni kutokana na utafiti uliofanyika katika shule zenye watoto viziwi ikiwemo Njombe viziwi ambao  ufaulu wao uliendelea kushuka.


Kilele cha maadhimisho ya wiki ya Viziwi duniani kitaifa yamefanyika mkaoni Tabora ikiwa ni hatua ya kuenzi historia ya chimbuko la elimu kwa viziwi kwani shule ya kwanza ya viziwi nchini Tanzania ilianzishwa katika mkoa huo.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: