Tuesday, 25 August 2020

WATEULE WA VYAMA 6 VYA SIASA WATANGAZWA KUINGIA KWENYE KINYANG'ANYIRO CHA UBUNGE ARUMERU MAGHARIBI


Msimamizi wa Uchaguzi, Jimbo la Arumeru Magharibi, Saad Mtambule, ametangaza majina ya Uteuzi wa Ubunge Jimbo hilo, uteuzi uliofanyika kwa mujibu ya ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuanzia tarehe 12- 26 Agosti, 2020 saa kumi kamili Jioni.

   Msimamizi huyo  wa Uchguzi amefafanua kuwa, jumla ya Wateule wa Ubunge 12 kutoka vyama 12 vya siasa, walichukua fomu za Uteuzi katika Jimbo hilo na baadhi yao, kuzirejesha fomu hizo kwa wakati kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizotolewa nanTume ya Taifa ya Uchaguzi.

    Kati ya Wateule hao 12, wateule 6 wa vyama sita vya siasa walikidhi vigezo na kuteuliwa huku wateule 3 wa vyama vitatu vya siasa waliorejesha fomu hawakukidhi vigezo na kushindwa kuteuliwa.

     Aidha amewataja Wagombea walioteuliwa ni pamoja na Mch. Laiser Loilile Wison wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Tumaini Andrea Akyoo wa chama cha  UPDP,  Noah  Lembris Saput Mollel wa Chama cha Mapinduzi- CCM,  Lairumbe John Kivuyo wa Chama cha ACT- Wazalendo, Gibson Ole Mesaiyek wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo - CHADEMA  na  Arafa Mohamed Muya wa Chama cha Wananchi CUF.

    Hata hivyo amewataja Wateule ambao walichukua fomu na kuzirejesha lakini hawakukidhi vigezo vya kuteuliwa ni pamoja na Ramadhani Lila Msoma wa chama cha AAFP, Elias Fatael Chonjo wa Chama cha Sauti ya Umma - SAU na Frida Marko Nnko wa chama cha UMD.

    Wateule amabao walichukua fomu za Uteuzi wa Ubunge na hawakuzirudisha  kwa Msimamizi wa Uchaguzi ni pamoja na Mteule wa Chama cha Demokradia Makini, Chama cha Jamii - CCK na Chama cha ADC- Dira ya Maendeleo.

     Msimamizi huyo wa Uchaguzi, ametangaza ratiba ya Kampeni za Uchaguzi kuanza rasmi kesho tarehe 27 Agosti mpaka tarehe 27 Oktoba, 2020 na kuwataka wagombea wote walioteuliwa, kufanya kampeni za kistaarabu na kupepuka lugha za kejeli na matusi huku akiwasisitiza  wananchi kwenda kwenye mikutano ya kampeni na kusikiliza sera za wagombea ili kuchagua viongozi bora siku ya Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ifikapo ya tarehe 28 Oktoba 2020.

No comments:

Post a Comment