Chini ya asilimia 10 ya nchi zina sheria zinazosaidia kuhakikisha ujumuishaji kamili katika elimu, kwa mujibu wa Ripoti ya Dunia ya Ufuatiliaji wa Elimu 2020: Ujumuishaji na Elimu – Tukisema wote, Basi ni Wote, kutoka UNESCO.

Ripoti hii inatoa uchanganuzi wa kina kuhusu vipengele msingi vya utengaji wa wanafunzi katika mifumo ya elimu ulimwenguni vikiwemo mahali walimotoka, utambulisho na uwezo (yaani, jinsia, umri, mahali walimotoka, umaskini, ulemavu, kabila, asili, lugha, dini, hali ya uhamiaji au ufurushwaji, mwelekeo wa kingono au utambulisho wa kijinsia, kufugwa jela, imani na mitazamo).

Ripoti hii imetambua kuwa utengaji umeongezeka wakati huu wa janga la COVID-19 na kukadiria kuwa karibu asilimia 40 ya nchi za kipato cha chini na cha kati hazitoi usaidizi wowote kwa wanafunzi walio katika hali ngumu wakati huu ambapo shule zimefungwa kwa muda.

Ripoti ya Dunia ya Ufuatiliaji wa Elimu 2020 inahimiza nchi ziwazingatie walioachwa nyuma shule zinapofunguliwa ili kujenga jamii thabiti na zenye usawa zaidi.

“Ili kukabiliana na changamoto zinazotukumba, ni muhimu tulenge kufikia elimu jumuishi”, alisema Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay. “Umuhimu wa kufikiria upya mustakabali wa elimu unadhihirika zaidi kufuatia janga la COVID-19, ambalo limepanua zaidi na kuangazia ukosefu
wa usawa. Kutochukua hatua kutazuia jamii kusonga mbele.”

Utengaji bado upo: Ripoti ya GEM ya mwaka huu ni ya nne katika msururu wa ripoti za UNESCO ambazo zinafuatilia hatua zilizopigwa na nchi 209 katika kutimiza malengo ya elimu yaliyopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. Ripoti hii
imesema kuwa watoto na vijana milioni 258 hawapati elimu yoyote, sababu kuu ikiwa umaskini.


Katika nchi za kipato cha chini na cha kati, vijana kutoka asilimia 20 ya familia tajiri walikuwa na uwezekano mara tatu wa kukamilisha vidato vya chini vya sekondari ikilinganishwa na wale wa familia maskini. Miongoni mwa waliokamilisha vidato vya chini vya sekondari, ujuzi wa wanafunzi
kutoka familia tajiri wa hisabati na kusoma ulikuwa maradufu ule wa wanafunzi kutoka familia maskini. 


Licha ya lengo la kuhakikisha wanafunzi wote wanakamilisha vidato vya juu vya sekondari kufikia 2030, ni wanafunzi wachache sana wa kike kutoka vijijini waliokamilisha masomo ya sekondari katika angalau nchi 20, nyingi zikiwa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Aidha kulingana na ripoti hii, wanafunzi wa umri wa miaka 10 katika nchi za kipato cha kati na cha juu ambao walifundishwa kwa lugha nyingine kando na lugha yao asili kwa kawaida walipata alama asilimia 34 chini ya wazungumzaji asili katika mitihani ya kusoma. Katika nchi 10 za kipato cha chini na cha kati, uwezekano wa wanafunzi wenye ulemavu wa kupata ustadi wa kusoma ulikuwa chini kwa asilimia 19 ikilinganishwa na wa wale wasio na ulemavu. Kwa mfano nchini Marekani, kulikuwa na uwezekano mara tatu wa wanafunzi wa LGBTI kusema kuwa walikosa kwenda shule kutokana na
kutojihisi salama.

Misingi isiyo sawa: Pamoja na ripoti hii ya leo, timu ya UNESCO inayotoa Ripoti ya GEM pia ilizindua tovuti mpya, PEER, iliyo na maelezo ya sheria na sera za ujumuishaji katika elimu za kila nchi ulimwenguni. Tovuti ya PEER inaonyesha kuwa nchi nyingi bado zina ubaguzi katika elimu, jambo ambalo linaendeleza kasumba, ubaguzi na utengaji. Sheria katika robo ya nchi zote zinahitaji  watoto wenye ulemavu wapate masomo katika muktadha tofauti, idadi hii ikizidi asilimia 40 katika nchi za Amerika ya Latini na Karibi, pamoja na Asia.

Utengaji dhahiri: Nchi mbili barani Afrika zimepiga marufuku wasichana wenye mimba shuleni. Zingine 117 ziliruhusu ndoa za watoto, huku zingine 20 zilikuwa bado hazijapitisha Mapatano ya 138 ya Shirika la Kimataifa la Leba ambayo yanapiga marufuku utumikishaji watoto. Katika nchi kadhaa
za Ulaya ya kati na mashariki, watoto wa Roma walitengwa katika shule za kawaida. Barani Asia, wakimbizi kama wale wa Rohingya walisomea katika mifumo sambamba ya elimu. Katika nchi za
OECD, zaidi ya theluthi mbili za wanafunzi kutoka familia za wakimbizi walienda shule ambapo angalau asilimia 50 ya wanafunzi wote walikuwa wakimbizi, jambo ambalo lilipunguza nafasi yao ya kufaulu katika elimu.

“Ugonjwa wa COVID-19 umetupatia nafasi ya kuwaza upya kuhusu mifumo yetu ya elimu,” alisema Manos Antoninis, Mkurugenzi wa Ripoti ya Dunia ya Ufuatiliaji wa Elimu. “Lakini kufikia ulimwengu ambao unathamini na kukaribisha uanuwai hakutafanyika mara moja. Kuna mvutano dhahiri kati ya kuwafundisha wanafunzi wote pamoja na kubuni mazingira faafu kwa wanafunzi kusomea. 

Lakini ugonjwa wa COVID-19 umetuonyesha kuwa kuna nafasi ya kufanya mambo kwa njia tofauti, tukiwaza kwa pamoja.”

Ilidhihirika kuwa imani baguzi za wazazi zilikuwa kizuizi kwa ujumuishaji: Asilimia 15 ya wazazi nchini Ujerumani na asilimia 59 kule Hong Kong, Uchina walikuwa na wasiwasi kuwa watoto wenye ulemavu walikatiza masomo ya watoto wengine. Wazazi wenye watoto walio katika hatari ya
kuathirika walichagua kuwapeleka watoto wao katika shule ambazo zilihakikisha ustawi wao na kushughulikia mahitaji yao. Kule Queensland, Australia, asilimia 37 ya wanafunzi katika shule maalum walikuwa wametoka shule za kawaida.

Ripoti hii inaonyesha kuwa mara nyingi mifumo ya elimu hukosa kuzingatia mahitaji maalum ya wanafunzi. Ni nchi 41 pekee ulimwenguni zilizotambua lugha ya ishara na pia, ulimwenguni kote, shule zilikuwa na hamu zaidi ya kupata intaneti ikilinganishwa na kushughulikia wanafunzi wenye
ulemavu. Takriban wasichana milioni 335 walihudhuria shule ambazo hazikuwa na huduma na maji na usafi walizohitaji ili kuendelea na masomo wakati wa hedhi.

Kuwatenga wanafunzi: Wakati wanafunzi hawajawakilishwa kikamilifu katika mitaala na vitabu vya kusoma, wao huhisi kuwa wametengwa. Wanawake na wasichana huwa asilimia 44 pekee ya marejeleo katika vitabu vya Kiingereza vya sekondari nchini Malaysia na Indonesia, huku Bangladesh ikiwa na asilimia 37 na wilaya ya Punjab, nchini Pakistani ikiwa na asilimia 24 pekee.

Walimu wanahitaji na wanataka mafunzo ya ujumuishaji, ambayo chini ya mwalimu mmoja kwa kila walimu 10 wa shule za msingi katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, zinazozungumza Kifaransa, walisema kuwa wamepata. Robo ya walimu katika nchi 48 walisema kuwa wanahitaji
mafunzo zaidi ya jinsi ya kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Ukosefu uliokithiri wa data ya ubora wa juu kuhusu walioachwa nyuma. Karibu nusu ya nchi za kipato cha chini na cha kati huwa hazikusanyi data ya kutosha ya elimu kuhusu watoto wenye ulemavu. Tafiti zinazohusisha familia ni muhimu katika kuchanganua data ya elimu kwa misingi ya
sifa bainifu. 


Lakini asilimia 41 ya nchi – zenye asilimia 13 ya idadi ya watu ulimwenguni – hazikuwa zinafanya tafiti hizi wala hazikuwa na data kutoka tafiti kama hizo. Takwimu kuhusu masomo sana sana hutolewa shuleni, hivyo kutojumuisha wale ambao hawaendi shuleni.

“Kutokuwa na data ya kutosha kunamaanisha kuwa tuna sehemu kubwa ya taswira ambayo hatuioni,” anasema Antoninis. “Ndio maana tofauti zilizodhihirika wakati wa COVID-19 zilitupata bila
kutarajia.”

Dalili za maendeleo katika kufikia ujumuishaji: Ripoti hii na tovuti ya PEER zimetaja kuwa nchi nyingi zilikuwa zinatumia mbinu chanya na bunifu ili kufikia ujumuishaji. Nchi nyingi zilikuwa zinaanzisha vituo vya nyenzo kwa ajili ya shule nyingi na kuanzisha shule za kawaida zinazoweza kuwapatia nafasi wanafunzi wenye mahitaji maalum, kama ilivyo nchini Malawi, Cuba na Ukraini.

Nchi za Gambia, New Zealand na Samoa zilikuwa zinatumia walimu wa kuzungukazunguka ili kuwafikia wale wasiofikiwa na huduma.

Nchi nyingi pia zilionekana kujitahidi ili kushughulikia mahitaji tofauti ya wanafunzi: Kwa mfano, jimbo la Odisha nchini India lilitumia lugha 21 za makabila madarasani, nchi ya Kenya ikarekebisha mtaala ili kuambatana na kalenda ya jamii za wahamiaji na nchini Australia, mitaala ya asilimia 19
ya wanafunzi ilirekebishwa na walimu ili matokeo yaliyotarajiwa yaambatane na mahitaji ya wanafunzi.

Ripoti hii inajumuisha nyenzo za kampeni dijitali, Tukisema Wote, Basi ni Wote, ambayo inaendeleza kundi la mapendekezo muhimu katika kipindi cha miaka kumi ijayo
Share To:

Post A Comment: