Saturday, 27 June 2020

Meneja Bandari ya Kipumbwi ashikiliwa kwa rushwa

Na Hadija Bagasha,  Tanga
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tanga inamshikilia Meneja wa Bandari ya Kipumbwi iliyopo Wilayani Pangani Mkoani Tanga, Steven Mbakweni kwa kosa la kuomba na kushawishi hongo ya Sh. 900,000 kutoka kwa mteja wake ili aweze kumruhusu kusafirisha mzigo wake kutoka Pangani kwenda Zanzibar kupitia bandari hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa yake, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Antony Gangolo imeeleza kuwa, katika uchunguzi uliofanywa taasisi hiyo ilibaini kuwa, meneja huyo aliomba na alishawishi hongo hiyo ikiwa ni baada ya mteja huyo kumpatia nyaraka zote zinazohitajika ambazo zilitolewa na ofisi ya bandari Pangani mjini zilizoonesha kuwa mteja huyo kufanya malipo na kutekeleza taratibu zote zinazotakiwa na zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ili aweze kusafirisha mzigo wake kwenda Zanzibar kupitia bandari hiyo ya kipumbwi.
Licha ya kuwa na kila kitu lakini nyaraka hizo zilikataliwa na meneja huyo kwa madai kwamba hazitambui huku akiwa na lengo la kushawishi apewe hongo ya sh. 900,000 ili aweze kuruhusu mzigo huo usafirishwe kupitia bandari hiyo.
Amesema, baada ya kupokea taarifa ya tuhuma hizo walianza kufanya uchunguzi na ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kuweka mtego wa rushwa ambapo mtuhumiwa huyo alikamatwa katika bandari ya Kipumbwi akiwa amepokea rushwa ya sh. 270,000 ambayo alikubali kuipokea kama hongo baada ya mteja huyo kumbembeleza ili ampunguzie.
”Kitendo hiki ni kosa chini ya kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana ma rushwa namba 11 ya mwaka 2007 tumemkamata na tunamshikilia Stephen Mbakweni kwa tuhuma za kuomba na kushawishi hongo atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili,”amesisitiza Naibu mkuu huyo.
Hata hivyo taasisi hiyo imetoa onyo kwa watumishi wa umma na watu wote wenye tabia ya kufanya vitendo vya rushwa kwani hawatasita kuwachukulia hatua za kisheria na kuwaasa wale wote wenye tabia hizi waache mara moja na wafanye kazi kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu.
Aidha amewaasa na kuwahimiza wadau na wananchi wa Mkoa wa Tanga kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa hususani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
”Niwasihi wananchi wote wa Mkoa wa Tanga kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa ili kwa pamoja tuweze kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha kwamba viongozi waadilifu ndio wanapewa dhamana ya kuongoza kwa ridhaa ya wapiga kura,” amesema Naibu mkuu huyo.

No comments:

Post a Comment