Friday, 13 March 2020

KANISA PENTEKOSTE LAWAPA NENO WAGOMBEA UCHAGUZI MKUU.......

Askofu Mkuu wa Kanisa la FPCT, Stevie Mulenga akimsimika mmoja wa Maaskofu wapya kwenye Viwanja vya Kanisa hilo Kibaoni mjini Singida.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo akitoa salamu za Serikali kwenye Ibada ya kuwasimika Maaskofu 24 wa Kanisa hilo mjini Singida.
.......................... ..............
Na Abby Nkungu, Singida.
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (FPCT), Stevie Mulenga amewaasa Watanzania watakaogombea nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, kuhakikisha wanajiandaa kisaikolojia zaidi katika kupokea matokeo ya uchaguzi huo.

Askofu Mkuu Mulenga alitoa rai hiyo wakati wa Ibada maalum ya kuwasimika na kuwabariki Maaskofu 24 kutoka Majimbo mbali mbali nchini iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la FPCT Kibaoni mjini Singida.

Alisema kuwa katika mchakato wowote wa Uchaguzi, mwisho wa yote huwa kuna kushinda na kushindwa; hivyo wagombea watakaoshindwa waridhike na matokeo yao vinginevyo wanaweza kusababisha fujo na vurugu; vitendo ambavyo havina maslahi kwa Taifa hili.

“Mgombea hana budi kutambua kuwa nafasi ya uongozi anayowania iwe ya  Udiwani, Ubunge au Urais, inahitaji mtu mmoja tu. Akichaguliwa huyo  mmoja, biashara imeisha. Waliokosa wanapaswa kujipanga upya kwa uchaguzi ujao” alifafanua.

Kadhalika, aliwataka wagombea watakaoshinda kuhakikisha wanatumikia nafasi zao kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili Tanzania iweze kusonga mbele.

Akitoa ujumbe kwa Maaskofu waliosimikwa na waliobarikiwa, Askofu Mulenga aliwaagiza kufanya kazi zao kwa uadilifu kwa kushirikisha wake zao katika majukumu  yote ya kumtumikia Mungu.

Akitoa mfano wa njiwa na kunguru kutoka Kitabu cha Mwanzo katika Biblia Takatifu enzi zile za gharika, Askofu Mkuu huyo aliwaambia wahusika wasije kuwa kama kunguru aliyetumwa na Nuhu kwenda kuangalia iwapo maji yamepungua huko nje lakini asirejee kamwe;  bali wawe kama njiwa aliyepeleka mrejesho wa jani bichi la mzeituni likiwa kinywani mwake.

"Vivyo hivyo, nanyi mliosimikwa leo, mrejesho wenu kwa tendo hili la leo ni kwenda kuvuna waumini wa kutosha. Njiwa hufanya kazi kwa ushirikiano na mwenzi wake. Hutaga mayai mawili. Wakati wa kuatamia, huachiana zamu. Jike likishikwa na njaa humwachia njiwa dume kuatamia mayai” alisema na kuongeza;

Ninyi mliosimikwa leo, kafuateni utamaduni huu mzuri wa  njiwa. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na Maaskofu waaminifu na wenye mioyo safi isiyoyumbishwa na tamaa za dunia hii; hasa nyakati hizi ambapo kuna majaribu mengi ndani ya makanisa yetu".

Askofu Mkuu mstaafu, David Batenzi  alikemea vikali vitendo vya ndoa za jinsi moja, kufunga ndoa na mama mzazi au baba mzazi na binadamu kufunga  ndoa na mnyama akisema maasi ya aina hiyo ndiyo hasa yanayosababisha Yesu kuchelewa kurudi tena duniani.

“Nawasihi wananchi wote kupiga vita maasi haya kwa kuwa hayapendezi mbele ya jamii na ni chukizo machoni pa Mungu” alisema.

Naye, Mkuu wa mkoa wa Singida Dk Rehema Nchimbi aliwataka wanawake kutojinyanyapaa badala yake watekeleze kwa vitendo usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50.

Hata hivyo, alisema usawa huo wa kijinsia lazima uzingatie upendo na wala usiondoe dhana ya kujali malezi ya watoto wetu.

“Akinamama hamna budi kushika neno la Mungu, Ukiwa na Mungu, utamlea mwanao kwa njia ipasayo. Tunakuwa 'bize' hadi tunashindwa kuwalea watoto wetu katika njia ifaayo” alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Aidha, Dk Nchimbi aliligeukia Kanisa na kuwataka Viongozi wake kuhakikisha wanasaidia kwa vitendo malezi ya watoto. “Ni kweli tunataka 50 kwa 50 pia tunataka usawa wa kijinsia lakini tusaidieni katika kukemea roho ya ulawiti, kubaka na utumiaji madawa ya kulevya”. MWISHO  No comments:

Post a comment