Katika kusaidia kuwezesha Vijana kushiriki kikamilifu kwenye Ujenzi wa Uchumi wa Taifa na kutatua tatizo l Ajira,Serikali ya Awamu ya Tano Chini ya Mh Rais Dr John Pombe Joseph Magufuli inatekeleza mkakati wa kuwajengea Vijana Ujuzi katika eneo la Utalii na Ukarimu ili kuongeza ushiriki mkubwa wa Vijana katika sekta hiyo yenye mchango mkubwa kwenye pato la Taifa.

Hayo yamesemwa leo Wilayani Chato na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde wakati akikabidhi mkopo wa Tsh 92,000,000 kwa Vikundi vya Vijana wa Mkoa wa Geita uliotolewa na Mfuko wa Maendeleo Vijana ambapo jumla ya Vikundi 12 kutoka Mkoa wa Geita vimenufaika,na kuwataka Vijana hao kutumia mkopo huo kama mtaji wa kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuhakikisha wanarejesha ili Vijana wengine waweze kukopeshwa pia.

"Katika Programu zetu za kukuza ujuzi sasa tutaliangalia eneo la Utalii na Ukarimu ili kuwajengea uwezo vijana kwa idadi kubwa kuwa mstari wa mbele kuchangamkia fursa za Utalii kupitia mafunzo mbalimbali ya vitendo kwa kushirikian na wadau wa sekta ya utalii,hapa mna Mbuga ya Wanyama ya Burigi-Chato vijana msikae nyuma kuchangamkia fursa ili kujiongezea kipato na kutatua changamoto ya Ajira"Alisema Mavunde

Naye Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri Wa Nishati Dr. Medrad Kalemani ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uwezeshwaji wa wakina mama na Vijana katika wilaya ya Chato hali iliyopelekea kuongezeka kwa shughuli nyingi za kiuchumi na hivyo kutatua matatizo ya kipato kwa wananchi hao kwa kiasi kikubwa.

Akitoa salamu zake kwa Vijana,Mbunge wa Geita Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mh Constantine Kanyasu amewataka Vijana kutumia mkopo huo kama ngazi ya kufikia mafanikio yao ya kujikwamua kiuchumi na kuahidi Wizara yake kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kusimamia mafunzo ya Utalii na ukarimu kwa Vijana ili kushiriki kwa ukamilifu kwenye sekta ya Utalii ambayo kwa hivi sasa bado kuna mahitaji makubwa ya nguvu kazi yenye ujuzi stahiki
Share To:

msumbanews

Post A Comment: