Saturday, 14 December 2019

RC Gambo awataka Makamanda wa Polisi kuja na mbinu za kisasa kukabiliana na Uhalifu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amewataka Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini kuja na mikakati na mbinu za kisasa katika kukabiliana na matukio ya uhalifu.


Ameyasema hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Makamanda wa Polisi kanda ya Kaskazini ambacho  kinahusisha Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara kilichofanyika katika ukumbi wa bwalo la Maofisa wa Polisi Jijini Arusha.

Amesema pamoja na Jeshi hilo kufanya kazi nzuri, amewataka Makamanda hao kujadili na kuweka mikakati  mipya na ya kisasa ambayo itawezesha katika kukabiliana na matukio ya uhalifu na wahalifu hususani mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, Uhalifu unaovuka mipaka, Ulinzi wa Madini na kuweka mazingira mazuri ya kiusalama kwa sekta ya utalii.

‘‘Makamanda shirikishaneni mbinu za kisasa za kukabiliana na uhalifu, kwa sababu Wahalifu hawatakuwa na sehemu ya kukimbilia kwa kuzingatia maeneo yote katika kanda hii ya kaskazini mbinu za kihalifu zinafanana’’. Alisema Gambo.

Naye Kamishna wa Polisi Intelijensia ya Jinai CP. Charles Mkumbo ambaye pia ni Mlezi wa Kanda hiyo amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuweka mikakati ya pamoja katika kuhakikisha Kanda hii inaendelea kuwa shwari hasa kwa kuzingatia kanda hii ni kitovu cha utalii hapa nchini.

‘‘Nimekuja ili kuhakikisha Makamanda hawa wanaungana pamoja, Kama ni msako ufanyike kwa siku moja katika mikoa yote ili kuhakikisha wahalifu wanakosa sehemu ya kujificha’’. Alisisitiza Kamishna Mkumbo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga alisema wamekutana ikiwa ni utaratibu wao wa kukutana kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kukabiliana na uhalifu.

Aliongeza kwa kusema kuwa watajadili na kuweka mikakati ambayo watakuja na maazimio ya pamoja ya kukabiliana na Matukio yote ya kihalifu hasa katika maeneo ya mipaka ya Namanga, Holili, Hororo na Tarakea ili kuhakikisha Wahalifu wanakosa sehemu ya kukimbilia.

No comments:

Post a comment